Home LOCAL JAFO: WOTE WALIOVAMIA VYANZO VYA MAJI WAONDOKE MARA MOJA.

JAFO: WOTE WALIOVAMIA VYANZO VYA MAJI WAONDOKE MARA MOJA.

Na. Jacob Kasiri -Ruaha.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb) amewataka wananchi wote waliovamia bonde la Ihefu ambalo ni chanzo cha mto Ruaha Mkuu kuondoka mara moja ili kuondokana na athari zilizopelekea mto Ruaha Mkuu kutotiririsha maji kwa miezi mitatu mfululizo.

Ameyasema hayo leo katika kikao kilichowahusisha Mawaziri nane wa Kisekta, Makatibu wakuu, wakuu wa Mikoa pamoja na
wataalam kilichofanyika katika Hifadhi ya Taifa Ruaha iliyoko mkoani Iringa.

“Wale wote waliovamia vyanzo vya maji tumeazimia waondoke haraka iwezekanavyo, swala la kuondoka halina mjadala wa kusubiri mwezi au miezi miwili. Mara baada ya kikao hiki cha leo Novemba 15, 2022 wote waliovamia vyanzo vya maji na kusababisha uharibifu mkubwa mnatakiwa kuondoka mara moja. Hii kauli tukisema mara moja ni kuanzia leo,” amesisitiza Waziri huyo.

Waziri Jafo ametaja sababu za kukauka kwa mto Ruaha Mkuu ni pamoja na uingizaji wa mifugo ndani ya bonde la Usangu na kwenye ardhi oevu ya Ihefu, uchepushaji wa maji toka kwenye mito inayoingiza maji bonde la Usangu unaofanywa na baadhi ya wakulima wasiofuata sheria na taratibu pamoja na ukataji na uchomaji wa misitu unaosababisha ukame na uharibifu wa mazingira.

Eneo la darajani ambalo Mawaziri, wakuu wa Mikoa na wataalamu hao wamelitembelea ni moja ya kivutio ndani ya hifadhi hii pindi mto Ruaha Mkuu unapokuwa unatiririsha maji yake ambapo watalii hushuka na kupiga picha mbalimbali kutokana na mandhari nzuri ya beta (meanders) za mto huo, sasa hivi yamesalia madimbwi yenye maji machache na machafu yanayopelekea maisha ya viboko, mamba, samaki na wanyama wengine wanaotegemea maji hayo kuwa hatarini.

“Mambo ya haraka ili kunusuru hali hii ni pamoja na Mamlaka ya bonde za maji kusimamia sheria iliyopitishwa na Bunge 2022 inayoelekeza wale wote wanaochepusha maji kinyume cha sheria kuchukuliwa hatua. Pia naelekeza Mamlaka ya bonde za maji pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kubaini wale wote waliovamia vyanzo vya maji waondoke haraka”, aliongeza Waziri huyo.

Uhai wa hifadhi ya taifa Ruaha hutegemea mto Ruaha Mkuu, hivyo kukauka kwake hakutaathiri tu hifadhi hii katika shughuli za utalii na uhifadhi bali pia itaathiri shughuli za kiuchumi kama vile uzalishaji wa umeme, kilimo na uvuvi unaofanyika katika bwawa la Mtera. Kama tujuavyo zaidi ya asilimia 65 ya umeme unaozalishwa kwa njia ya maji nchini Tanzania hutegemea maji yanayotokea bonde la Ihefu kupitia mto Ruaha Mkuu.

Previous articleRAIS MHE.SAMIA SULUHU HASSAN APOKEAHATI ZA UTAMBULISHO ZA MABALOZI 6 WANAOWAKILISHA NCHINI ZAO HAPA TANZANIA, IKULU CHAMWINO, DODOMA 
Next articleMAKAMU MWENYEKITI WA CTI HUSSEIN SUFIAN AZUNGUNZIA TUZO ZA RAIS KWA MZALISHAJI BORA WA MWAKA (PMAYA) KWA WAANDISHI WA HABARI JIJINI DAR
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here