Kutoka Dodoma Tarehe 18 Novemba, 2022
Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya Dkt. Beatrice Mutayoba amewasihi Uongozi na Walimu wa Shule ya Msingi Mtumba kuilinda na kuitunza miundombinu ya maji na vyoo iliyojengwa shuleni hapo.
Akizindua vyoo vya kisasa katika Shule ya Msingi Mtumba iliyopo katika kata ya Mtumba Halmashauri ya Jiji la Dodoma Dkt. Beatrice amesema miundombinu hiyo imejengwa kwa fedha nyingi, uongozi uhakikishe hakuna mtu anayekuja kufanya uharibifu wa aina yoyote ili iwe ni shule ya mfano.
“Kwa upande wa Walimu, ni imani yangu mmejipanga vyema kabisa kuhakikisha kunakuwepo na matumizi endelevu ya miundombinu hii na kwamba wanafunzi wanaelimishwa jinsi ya kuitumia” Amesema Dkt. Beatrice.
Pia Dkt. Beatrice amesema uwepo wa miundombinu bora na ya kisasa ya maji na choo katika shule ni kichocheo kimojawapo cha wanafunzi kufanya vizuri mashuleni.
“Tafiti zinaonesha kuwa, shule zenye miundombinu bora ya maji na usafi wa mazingira hupelekea wanafunzi kutumia muda mrefu zaidi shuleni ikilinganishwa na shule ambazo hazina miundombinu hivyo kupelekea wnafunzi kufanya vizuri”.
Aidha, Dkt. Beatrice ametoa rai kwa wadau mbalimbali wa Afya na Elimu nchini kutumia vyoo hivyo kuwa ndio mfano pale ambapo wanapanga kujenga vyoo shuleni.
“Vyoo hivi vimezingatia mahitaji ya makundi yote wakiwemo Watumishi, Wanafunzi wenye ulemavu, wanafunzi wa kike pamoja na wavulana, pia kuna miundombinu inayowezesha unawaji wa mikono kwa pamoja bila kusahau uwepo wa kiteketezi kwa ajili ya kuchomea taulo za kike zilizotumika” Amesema Dkt. Beatrice.
Miundombinu iliyojengwa katika shule hiyo ni pamoja na matundu 11 ya vyoo vya kiume, matundu 10 ya vyoo vya kike, tundu 1 kwa ajili ya waalimu wa kiume, Tundu 1 kwa ajili ya walimu wa kike, sehemu ya kukojolea wanaume, chumba cha mahitaji maalum kwa wanafunzi wa kike, Tanki kubwa la kuhifadhi maji la lita 45,000, tanki kubwa la kusambazia maji la lita 10,000, sehemu 2 za kunawia mikono kwa makundi, Kichomea taka, choo cha walemavu na bomba 1 la kuchotea maji.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mtumba Mwl. Edward Maboje ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais Tamisemi na Mfuko wa Kimataifa wa Watoto (UNICEF) kwa namna ushirikiano wao umewezesha kukamilika kwa mradi huo mkubwa na wa mfano shuleni hapo.