Home LOCAL DKT. TAX AWAASA VIJANA KUIGA FALSAFA ZA UONGOZI WA NYERERE

DKT. TAX AWAASA VIJANA KUIGA FALSAFA ZA UONGOZI WA NYERERE

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amewaasa vijana kutumia vyema Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation kujifunza, kubadilishana mawazo juu ya falsafa za Mwalimu Nyerere pamoja na kuimarisha amani na umoja katika jamii.

Dkt. Tax ametoa wito huo alipokuwa akifungua mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation kwa kundi la kwanza la viongozi vijana 60 kutoka nchi zaidi ya 40 Barani Afrika tarehe 25 Novemba, 2022 usiku Jijini Dar es Salaam. Pamoja na mambo mengine, Dkt. Tax aliwasisitiza vijana hao kutumia mafunzo hayo kuinufaisha jamii inayowazunguka.

“Napenda kutumia fursa hii kuwasihi vijana wa kizazi kipya cha Viongozi wa Afrika na watu wa Afrika, kufanya kazi kwa umoja, ushirikiano, na imani thabiti, kwani bila kufanya hivyo ni vigumu kuwa na mustakabali wa Afrika tunayoitaka,” alisema Dkt. Tax.

Dkt. Tax aliongeza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi Imara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, imejipanga kuhakikisha vijana wanawezeshwa ili kuendeleza amani, usalama na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Katika kuenzi mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere katika kukuza umoja, amani na maendeleo ya watu nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla, Serikali inaendelea kuunga mkono mipango ya amani kwa kuchangia Misheni za ulinzi wa amani Barani Afrika na Kikanda. Leo hii Tanzania ni nchi ya 13 kwa ushiriki katika Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa Duniani,” aliongeza Dkt. Tax

Bara la Afrika limebarikiwa rasilimali nyingi, tuchanganye maarifa, ujuzi wa uongozi, na maliasili ilizonazo ili kupeleka bara la Afrika katika ngazi za juu zaidi. Kwa kufanya hivyo, vijana mtakuwa mmeenzi falsafa za uongozi za Mwalimu Nyerere, aliyeongoza mapambano ya kupigania uhuru, umoja, na kujenga misingi imara ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Awali akizungumza kabla ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation, Bw. Joseph Butiku alisema kuwa programu ya Mafunzo ya Uongozi kwa Vijana yanayotolewa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere ni mpango unaolenga kushirikisha viongozi vijana katika kutoa mafunzo, changamoto, kufafanua na kubadilisha mtazamo wa kizazi kipya cha Afrika kuwa viongozi wanaowajibika, wanaojitolea na wapenda amani.

“Malengo ya taasisi yetu ni kutafiti na kueneza falsafa ya uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, amani, umoja na maendeleo ya watu. viongozi wazuri na wenye tija wa sasa na wa siku zijazo wa bara hili,” alisema Bw. Butiku.

Mafunzo hayo yametolewa kwa vijana 60 kutoka mataifa mbalimbali ambayo ni Botswana, Burundi, Cameroon, Djibouti, Misri, Ethiopia, Gabon, Guinea, Kenya, Libya, Liberia, Namibia, Nigeria, Rwanda, Sudani, Sudani Kusini, Afrika Kusini, Tanzania, Uganda, na Zambia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here