Home BUSINESS DKT.MPANGO: BoT HAKIKISHA TAASISI ZA FEDHA ZINAPUNGUZA RIBA

DKT.MPANGO: BoT HAKIKISHA TAASISI ZA FEDHA ZINAPUNGUZA RIBA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango (kushoto) akizungumza alipokuwa katika Banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati wa ziara yake ya kukagua mabanda ya washiriki katika Wiki ya huduma za kifedha iliyofanyika leo Novemba 24, 2022 katika viwanja vya Rock city Mall Jijini Mwanza. (katikati) ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florence Luoga, na (kulia) ni, Meneja wa Uhusiano wa Benki hiyo Victoria Msina.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango (kushoto) akimsikiliza Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florence Luoga, (katikati) alipokuwa akizungumza wakati ziara za Makamu wa Rais akipotembelea Banda hilo katika Wiki ya Huduma za Kifedha Jijini Mwanza. (kulia) ni, Meneja wa Uhusiano wa Benki hiyo Victoria Msina.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florence Luoga, (katikati)  mara baada ya kumaliza ziara yake fupi katika Banda la Taasisi hiyo.

  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ihakikishe taasisi za fedha hapa nchini kuanza kutoa mikopo yenye riba nafuu ili ziwafikie wananchi wengi hususani wakulima.

Dk Mpango ametoa maagizo hayo alipotembelea Banda la Taasisi hiyo katika hafla ya kufungua rasmi Wiki ya huduma za kifedha iliyofanyika leo Novemba 24, 2022 katika viwanja vya Rock city Mall Jijini Mwanza. 

Amesema kuwa taasisi za fedha hapa nchini  zimekuwa zikitoa riba kubwa  inayowaumiza wananchi jambo ambalo husababisha baadhi yao kushindwa kukopa.

Aidha ameelezea uwepo wa mwitikio mdogo wa mabenki katika kuvutia wananchi wenye kipato cha chini na kati kuweza kukopa, na kwamba ni vyema wakalitazama jambo hilo ikiwemo suala la zima la masharti ya mikopo hiyo.

“Kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikitoa rai kwa taasisi hizi za kifedha kupunguza riba ili kuwasaidia wananchi waweze kukopa ambapo kwa sasa wananchi wanakopeshwa kwa riba ya asilimia 9 pekee wakati wao wanaenda kukopa Benki Kuu kwa asilimia 3 kwa nini wasipunguze na kuweka uwiano sawa angalau ifike asilimia 5?,” amehoji Dkt Mpango.

Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florence Luoga amesema kuwa Benki hiyo tayari imeshaanza kushughulikia suala hilo ambapo pamoja na mambo mengine BoT kwa kushirikiana na TBA wameanza kuzipitia changamoto zilizopo zitakazopelekea kulegeza masharti ya mikopo katika taasisi za fedha,

Ameeleza kuwa baada ya Serikali kuanza kutoa vitambulisho vya Taifa (NIDA) wanakusudia kuanza kuvitumia katika kuwakopesha wananchi na kwamba kwa sasa wanaendelea kufanyia kazi changamoto zinazojitokeza kwenye sekta ya fedha kwa lengo la kuboresha utolewaji wa huduma hiyo hapa nchini.

“Tunaendelea kufanyia kazi changamoto zinazojitokeza kwenye sekta ya fedha lengo ni kuhakikisha inaboresha mazingira ya utolewaji wa mikopo hiyo ili wananchi wote wanaendelee kunufaika nayo” amesema Prof Luoga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here