Home LOCAL CHANGAMOTO UTATUZI MGOGORO BARABARA YA KIGAMBONI

CHANGAMOTO UTATUZI MGOGORO BARABARA YA KIGAMBONI

Na Mwandishi Wetu

SIKU chache baada ya Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kuweka wazi mchakato wa kumlipa fidia mwekezaji kampuni ya ASM (T) LTD maeneo ya Kimbiji ili kufungua barabara inayotumika na wananchi na wawekezaji wengine kufika kwenye maeneo yao, hatua hiyo sasa imebadilika na wanaopaswa kulipa fidia hiyo hi baadhi ya wananchi wanatakaochukuliwa maeneo yao kupisha barabara imefahamika.

Juzi uongozi wa Halmashauri hiyo wakiongozwa na mkuu wa Wilaya Fatuma Nyangasa, Mkurugenzi, Erasto Kiwale, madiwani wakiongozwa Meya wa Manispaa hiyo, walitembelea na kufanya ukaguzi kwenye eneo la mgogoro huo, Mikenge kata ya Kimbiji ambapo walikagua barabara iliyozuiliwa pamoja na maeneo yaliyopendekezwa na mwekezaji ASM kupitisha barabara mpya.
Wakizungumza na gazeti, baadhi ya wakazi ambao maeneo yao yatachukuliwa walisema wanashangazwa na maamuzi mapya ya Manispaa hiyo.

“Maamuzi tunayoyafahamu tangu hapo awali ni kulipwa fidia kwa huyu mwekezaji, viongozi juzi walikuja wakakagua nakuona kabisa makosa yaliyofanywa kufungwa barabara hii, tumeshangazwa sasa wanakuja kupima maeneo yetu ili wayachukue kupisha barabara wakati tayari huyu ASM alitakiwa kulipwa fidia ili abomoe ukuta wake kufungua barabara, hii imetushangaza sana, tunahoji nini huyu mwekezaji amewapa mpaka wanabadilisha maamuzi,” aliohoji Mzee mwenyepingu Mbwana aliyeishi maeneo hayo kwa zaidi ya miaka 30.

Aidha, mkazi mwingine Ramadhan Muro, alisema anashangazwa na maamuzi yanayotoka sasa ya kuchukua maeneo ya wananchi wakati barabara ya asili ilikuwepo.

” Wamekuja hapa na mimi nilikuwepo, wamejionea wepesi upo wapi, pingamizi ya barabara hii ni ukuta tu wa huyu mwenzetu ASM na uongozi wamekagua na kujionea, sasa haya maamuzi mengine mapya yametushangaza sana, hatuna nia ya kubishana na Serikali, lakini maamuzi haya yanatupa mashaka,” alisema Muro.

Mwenyekiti wa kijiji, Lameck Mayala, alisema maamuzi hayo mapya ya Manispaa yamewashangaza kwa kuwa baadhi ya wananchi wanyonge walioishi muda mrefu maeneo hayo watapoteza maeneo yao.

Wiki iliyopita akizungumza na gazeti hili, Kamishna msaidizi wa ardhi mkoa wa Dar es Salaam, Idrisa Kayela alisema mgogoro huo wa barabara ulidumu Kwa muda mrefu lakini wameshautatua kwa kuiagiza Manispaa ya Kinondoni kumlipa fidia mwekezaji ASM ili kuvunja ukuta kuruhusu barabara iliyoanzia barabara kubwa kuelekea kwenye fukwe na maeneo mengine kutumika.

Kamishna Kayela aliweka wazi kuwa tathmini ya awali kubaini gharama za fidia zilifanyika na ilibaki utekelezaji kwa Manispaa hiyo.Jana alipoulizwa Mkurugenzi wa Kigamboni, Erasto Kiwale juu ya kinachoendelea sasa, alikiri juzi kuwepo kwa ziara ya viongozi wa Manispaa hiyo kwenye eneo la mgogoro lakini hakutaka kuweka wazi maamuzi ya kikao kilichofanyika baaada ya ziara hiyo.

“Hiki ni kikao cha ndani, maamuzi yake hayajatoka na vikao vinaendelea, siwezi kusema lolote kwa sasa,” alisema Kiwale.
Hata hivyo wiki iliyopita, Kiwale alikiri kupokea maagizo kutoka ngazi za juu za kuwataka kumlipa fidia mwekezaji ASM ili barabara hiyo kufunguliwa.

Akizungumza wiki iliyopita ofisini kwake, Kiwale aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati Manispaa ikiendelea na taratibu zake za kiofisi za kumlipa fidia mwekezaji huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here