Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa Novemba 11, 2022 akiwaongoza Wajumbe wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi kuimba wimbo wa Mshikamano Daima unaowataka kuijunga kwa pamoja kwa maendeleo ya Taasisi
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa, amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kuhakikisha kuwa wanasimamia ipasavyo utendaji kazi pamoja na nidhamu ya watumishi ili kuongeza ufanisi wa Taasisi.
Bw. Nyaisa ametoa agizo hilo Novemba 11, 2022 wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi kinachofanyika mkoani Morogoro.
Bw. Nyaisa amesema kwakuwa Baraza la Wafanyakazi ni chombo cha ushirikishaji wa watumishi na linaundwa na wajumbe kutoka Menejimenti ya BRELA, viongozi wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) na wawakilishi wa watumishi kutoka idara mbalimbali, wajumbe wote wanao wajibu wa kusimamia utendaji kazi pamoja na nidhamu ya watumishi ili kutoharibu taswira ya Taasisi.
Bw. Nyaisa amesema pia viongozi wa TUGHE kama wajumbe wa Baraza wanapaswa kufuatilia maslahi ya wafanyakazi kwa kushirikiana na Menejimenti, hivyo wanapoona kuna jambo lolote ambalo haliendi sawa wanapaswa kutoa taarifa mapema.
“Siyo jambo jema kwa viongozi wa TUGHE kukaa kimya kwa mambo ambayo yako wazi na kusubiri Menejimenti ya Taasisi ndiyo afuatilie,”amesisitiza Bw. Nyaisa.
Akizungumzia umuhimu wa Vikao vya Baraza Bw. Nyaisa amesema, vikao vinasaidia kutatua changamoto za wafanyakazi kwa uwazi na kuondoa manung’uniko ambayo yanaweza kujitokeza.
Pamoja na mambo mengine Baraza la wafanyakazi hukutana mara 2 kila mwaka, kuidhinisha mipango na bajeti ya wakala pamoja na kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa malengo ya wakala kwa mwaka.