Home LOCAL ASILIMIA 95 YA MAGONJWA YA KUAMBUKIZWA NI KUTOTUMIA HUDUMA ZA MAABARA

ASILIMIA 95 YA MAGONJWA YA KUAMBUKIZWA NI KUTOTUMIA HUDUMA ZA MAABARA

* 90% ya wafugaji wanatumia dawa za antibiotiki kutibuW anyama badala ya chanjo.

Na. Catherine Sungura, WAF-Dodoma

Tanzania inakabiliwa na magonjwa ya kuambukizwa kwa asilimia 95 kutokana na baadhi ya watumishi kutopenda kutumia huduma za maabara hali hiyo imesababisha wagonjwa wengi wamekuwa wakitibiwa bila kupata uhakiki wa majibu kutoka maabara huku 90% ya wafugaji wanatumia dawa za antibiotiki kutibu Wanyama badala ya chanjo.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu, wizara ya Afya Dkt. Seif shekalaghe wakati akitoa tamko la Wiki ya kampeni ya kuzuia usugu wa Vimelea dhidi ya dawa za Antibiotiki inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 18-24 Novemba ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kwa Pamoja tuzuie usugu wa vimelea dhidi ya dawa”.

Dkt. Shekalaghe amesema kuwa hali hiyo imepelekea matumizi yasiyo rasmi ya antibiotiki ambayo husababisha usugu wa vimelea kuongezeka mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 1993 matumizi yalikuwa (39%), mwaka 2002( 42%), 2014( 67.7%) na 2017 hadi 2022 wastani wa (65%).

“Matokeo ya tafiti iliyofanyika mwaka 2017 yalionesha kwamba 92% ya wagonjwa hupata matibabu yao katika maduka ya dawa na famasi na kati yao 92.3% hununua antibiotiki holela bila kutumia cheti cha dawa kilicho idhinishwa na daktari, kwa takwimu hizi tunahitaji kufanya juhudi za makusudi kujinasua “.

“Utafiti uliofanyika mwaka 2018 ulionesha kwa 90% ya wafugaji wanatumia dawa za antibiotiki kutibu Wanyama badala ya chanjo, ukiangalia twakwimu hizi ni kiashiria tosha kwamba ongezeko la usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni mkubwa” Aliongeza Dkt. Shekalaghe.

Aidha, amesema usugu wa vimelea dhidi ya dawa unatuweka katika mashaka makubwa ya kupoteza nguvu kazi ya Taifa kwa kusababisha vifo kutokana na kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyotibika kwa kutumia dawa tulizonazo, kuongezeka kwa umaskini kutokana na kuugua kwa muda mrefu na kutumia dawa za ghali zaidi, na pia kuongezeka kwa vifo vya mifugo na uzalishaji hafifu wa chakula, na pia kuigharimu nchi mamilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumika kuliletea Taifa maendeleo.

Hata hivyo alisema Ripoti iliyotolewa na Benki ya Dunia mwaka 2017, imeonesha kuwa ifikapo mwaka 2050 uchumi wa Dunia utapungua kwa asilimia (3.8%) na kwamba kiasi cha dola za Marekani trilioni 3.4 zitapotea ifikapo mwaka 2030 kutokana na tatizo hilo “nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania zinaathirika zaidi ambapo kiasi cha dola za Marekani bilioni tisa (9) zitatumika kila mwaka kupambana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa hizo”.

“Jambo la kuzuia usugu ni letu sisi sote, hivyo kwa pamoja sekta zote ikiwemo Afya, Mifugo,Uvuvi, Kilimo na Mazingira, tuungane katika kuhakikisha tunapunguza au kuzuia usugu wa vimelea dhidi ya dawa,dawa sahihi inatolewa na kutumika tu pale inapohitajika. Pia niwakumbushe wananchi umuhimu wa kujikinga na maradhi kwa njia rahisi na ambazo zimehakikiwa kuwa zinafanya kazi.

Hata hivyo ameelekeza taasisi na vituo vyote vya kutolea huduma za afya kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kupambana na Usugu wa Dawa dhidi ya vimelea mbalimbali antimicrobial (2023-2028) na kuwaagiza Matabibu (prescriber) kote nchini, kuandika dawa kwa kufuata mwongozo wa matibabu wa mwaka 2021 na kutumia majina halisi ya dawa (generics) na kwa usahihi.Vile vile amewataka watoa dawa (Dispenser) kusoma na kuelewa maelekezo ya matabibu na kutoa maelekezo sahihi kwa wagonjwa.

Naye, Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw. Daudi Msasi ametaka dawa zitolewe kwa kufuata cheo cha dawa na kuongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya inahuisha mwongozo wa matibabu kila baada ya miaka mitatu ili kusaidia matibabu sahihi kwa wananchi na kuondoa dawa zilizojenga usugu wa dawa.

Previous articleJKCI YATOA MILIONI 180 MATIBABU YA WAGONJWA 12 NJE YA NCHI
Next articleASILIMIA 95 YA MAGONJWA YA KUAMBUKIZWA NI KUTOTUMIA HUDUMA ZA MAABARA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here