Na. Majid Abdulkarim, WAF – Dar es Salaam
Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wametakiwa kujitokeza kushiriki kwa wingi katika Kampeni ya ugawaji wa Kingatiba ili kudhibiti Ugonjwa wa Matende na Mabusha (Ngirimaji) inatarajiwa kuzinduliwa tarehe 21- 25, Novemba mwaka huu katika Halmashauri za Temeke, Kinondoni na Jiji la Dar es salaam.
Wito huo umetolewa leo na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Ilala, Mhe. Ng’wilabuzu Ludigija wakati akifungua kikao kazi cha kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Dar es salaam kwa lengo la kuwajengea uwezo katika utekelezaji wa Kampeni ya ugawaji wa Kingatiba ya kudhibiti Ugonjwa wa Matende na Mabusha (Ngirimaji).
Mhe. Ludigija amesema tatizo la ugonjwa wa matende na mabusha bado upo katika halmashauri za Temeke, Kinondoni na Jiji la Dar es salaam, hivyo ni muhimu kwa kila mwananchi kushiriki kikamilifu ili kuongeza nguvu katika kutokomeza magonjwa hayo.
Aidha, ameitaka jamii kuachana na Imani potofu kuwa ugonjwa huo unawaathiri wanaume pakee bali unawahusu watu wa jinsi zote.
“Kumekuwa na dhana potofu kuwa ugonjwa huo unawaathiri wanaume pekee jambo ambalo sio kweli kwani ugonjwa huo unaathiri makundi yote mawili wanaume na wanawake na ndio maana tunasisitisha watu wote washiriki kikamilifu”, Ludigija.
Ludigija ametoa rai kwa viongozi wa dini katika halmashauri tajwa kushirikiana na watoa huduma kuhakikisha wanajipanga vyema kuanzia ofisi ya mganga mkuu wa mkoa ili halamshauri hizo tatu ziweze kuungana na halmashauri nyingine ambazo zimefanikiwa kutokomozea ugonjwa huo.
Aidha, Mganga mkuu wa mkoa, Dkt Rashid Mfaume amesema tangu mwaka 2017 hadi 2022 wamefanikiwa kupasua wagonjwa wa mabusha 3000 kati ya 4174 waliowalenga sawa na asilimia 75.
Dkt. Mfaume ameongeza kuwa katika kampeni hiyo lengo ni kuwafikia watu nane katika kila watu 10 na kuzifikia kata 76 kati ya 102 na mitaa 407 ndani ya halmashauri za Temeke, Kinondoni na Jiji la Dar es Salaam.
Pamoja na hayo amesema ili kufanikisha utekelezaji wa kampeni hiyo wameendelea na mchakato wa kutoa mafunzo kwa watendaji na wenyeviti wa serikali za mitaa ili wasaidie kuwatambua walioathirika na ugonjwa mabusha na matende na kuwaunganisha na huduma za matibabu kwa wakati.