Home LOCAL WAZIRI MKUU AWATAKA WATUMISHI WATIMIZE MATARAJIO YA RAIS SAMIA

WAZIRI MKUU AWATAKA WATUMISHI WATIMIZE MATARAJIO YA RAIS SAMIA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma watimize wajibu wao kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia wafanye pindi anapowateua ama kuwapa ajira.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuona watumishi wa umma mkiwatumikia Watanzania. Nenda kwa wananchi mkawasikilize. Huwezi kuwahudumia bila kuwasikiliza na huwezi kujua changamoto zao bila kuwasikiliza,” amesema.

Ametoa wito huo leo mchana (Jumatano, Oktoba 19, 2022) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa, wilaya na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba kwenye ukumbi wao mara baada ya kuzindua jengo la Halmashauri hiyo.

Amewataka viongozi na watumishi hao wafanye kazi kwa kulenga matokeo. “Nataka tufanye kazi kwa matokeo, tufuate maelekezo na tuzingatie nidhamu. Tuna fedha za ndani na za Serikali Kuu. Tuzisimamie vizuri na naomba msijiingize kwenye matumizi mabaya ya fedha hizo,” aliwaonya.

Waziri Mkuu aliwapa mfano wa Mkuu wa shule ya sekondari Irugwa ambaye alipokea sh. milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa sita, lakini alizisimamia vizuri akamaliza madarasa, akajenga matundu matano ya vyoo, kuweka mfumo wa maji ya mvua na chenji iliyobakia akapiga lipu mabweni ya wasichana na kujenga mabafu licha ya kuwa shule iko kisiwani na kisiwa kiko mbali kutoka Nansio (makao makuu ya wilaya) na pia kiko mbali kutoka Mwanza ambako mahitaji yote yanafuatwa.

“Nanyi pia fanyeni hayo hapa Madaba, mtumishi wa umma jitahidi ufanye jambo ambalo wengine limewashinda. Mheshimiwa Rais Samia anatamani kuwa na watumishi wengi wa aina hiyo.”

Kuhusu hoja za CAG, Waziri Mkuu amesema Halmashauri hiyo ya Wilaya ilikuwa na hoja 46 ambapo hoja 28 zimefungwa na hoja 18 bado hazijafungwa. “Malizieni hoja hizi 18 zilizobakia,” amesisitiza.

Kuhusu ujenzi wa hospitali ya Halmashauri hiyo, Waziri Mkuu amewataka wakamilishe ujenzi kwa viwango alivyoviona na akampongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bw. Sajidu Mohammed kwa usimamizi mzuri.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here