Home BUSINESS “WATUMISHI WA MALIASILI WASIO WAADILIFU WAWAJIBISHWE”

“WATUMISHI WA MALIASILI WASIO WAADILIFU WAWAJIBISHWE”

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewaagiza Wakuu wa Wilaya nchini kuwawajibisha watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wasio waadilifu katika kusimamia maeneo ya Hifadhi.

Ameyasema hayo leo Oktoba 19, 2022 wakati wa Kikao cha Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ya kutatua migogoro ya ardhi katika vijiji 975 nchini, kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

“Niwaombe kama kisababishi cha uvamizi katika maeneo ya hifadhi ni watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mkuu wa Wilaya una nafasi ya kuwawajibisha kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii” amesema Mhe. Masanja.

Amewaelekeza viongozi wanaosimamia maeneo ya Hifadhi kushirikiana kwa pamoja katika utunzaji wa maeneo hayo bila kusubiria Wizara itatue mgogoro wa uvamizi.

Amefafanua kuwa kama watayasimamia vizuri maeneo yaliyohifadhiwa wananchi hawataendelea kuyavamia kwa sababu maeneo mengi yamevamiwa kutokana na viongozi wa eneo husika kuyaachia bila usimamizi wowote.

Mhe. Masanja amesisitiza kuwa maeneo yote yaliyohifadhiwa yanategemewa na Wizara nyingi zikiwamo Wizara ya maji, Wizara ya Madini na Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira hivyo wananchi wanapoyavamia maeneo hayo inaathiri utekelezaji wa majukumu ya wizara nyingine.

Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu idadi ya vijiji 920 nchini kuachiwa kwa wananchi kati ya vijiji 975 vilivyokuwa na migogoro ya ardhi ambapo vijiji 55 pekee vinaendelea kupatiwa ufumbuzi.

Katika jiji la Mwanza jumla ya vijiji 48 vina migogoro ya ardhi ambapo kati ya hivyo vijiji 14 viko katika Hifadhi ya Pori la Sayaka lililopo Wilayani Magu.

Vijiji hivyo vitaandaliwa mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuwafanya wananchi kuwa wahifadhi na walinzi wa hifadhi hiyo.

Previous articleMHE. SAMIA AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA MALKIA WA UHOLANZI
Next articleDKT. KIJAJI: MAPENDEKEZO UENDELEZAJI BANDARI YA BAGAMOYO KUFANYIWA KAZI KWA WAKATI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here