Home LOCAL WANAFUNZI WALIOSOMA RUVU SEKONDARI KUMUENZI MWALIMU NYERERE KWA KUCHANGIA UJENZI WA UZIO...

WANAFUNZI WALIOSOMA RUVU SEKONDARI KUMUENZI MWALIMU NYERERE KWA KUCHANGIA UJENZI WA UZIO WA SHULE HIYO

Na: Mwandishi Wetu.

WANAFUNZI waliosoma kwa nyakati tofauti Shule ya Sekondari Ruvu Mkoani Pwani iliyojengwa kwa msaada wa watu wa Cuba kupitia maombi ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wamesema wanatarajia kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuchangia Ujenzi wa uzio wa shule hiyo kupitia michango itakayotolewa na wanafunzi hao na wadau wa maendeleo.

Hatua hiyo inakuja kipindi hiki cha kumbukizi ya kufariki kwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambayo hufanyika kila ifikapo Oktoba 14 ya kila mwaka, hivyo wao wameamua kumuenzi kwa kuchangia Ujenzi wa uzio huo kwa kushirikisha wanafunzi waliosoma shuleni hapo tangu mwaka 1977 Shule hiyo ilipokuwa na Wanafunzi mchanganyiko ambayo kwa sasa kuna wanafunzi wa kike peke yake.

Wanafunzi hao kupitia taarifa yao kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Viongozi wao Veronica Chambuso, Noel Kiunsi na John Kitundu wamesema wanatambua mchango wa Mwalimu Nyerere kufanikisha kujengwa kwa shule hiyo, hivyo wao wanamuenzi kwa kuchangia Ujenzi wa uzio kwani ndilo hitaji kubwa la wanafunzi na walimu kwa sasa.

Akifafanua zaidi Katibu wa kundi la Wanafunzi hawa John Kitundu alisema Oktoba 22 mwaka huu wanatarajia kutembelea shule hiyo na kukabidhi Material ya Ujenzi wa Uzio huo kutoka kwa Wanafunzi hawa kwa Uongozi wa shule kwa ajili ya kufanikisha ujenzi huo na wanaamini kuna idadi kubwa ya waliosoma kwenye shule hiyo ambao wataguswa na kuchangia fedha, kokoto, mchanga na nondo kukamilisha Ujenzi huu.

“Wanafunzi ambao tumesoma shule ya sekondari Ruvu tumetafakari na kuona ni vema tukamuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa kurudisha shukrani zetu kwa kuchangia Ujenzi wa uzio wa shule hii, tumefikia uamuzi huu baada ya kuzungumza na Waalimu pamoja na Wanafunzi. Wanamahitaji mengi lakini kubwa zaidi ni uzio.Hivyo wanafunzi wote tuliosoma Ruvu kokote mlipo tunaomba ushiriki wenu kwenye kufanikisha jambo hili, ni la kujitolea lakini linamaana kubwa kwetu sote,”alisema Kitundu.

Aliongeza mbali ya wanafunzi, pia wanahamasisha Wazazi wa wanafunzi wa Shule ya sekondari Ruvu na wadau wengine kuungana kwa pamoja ili kufanikisha ujenzi wa uzio huo kwani unakwenda kuimarisha ulinzi na usalama wa wanafunzi mabinti wanaosoma hapo kwa sasa.

“Shule hii zamani ilikuwa mchanganyiko lakini kwa sasa wanasoma wasichana tu, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha watoto wetu wa kike wanaosoma shuleni hapo wanakuwa salama na hilo ni jukumu letu.Kwa wale ambao mioyo yao itaguswa na ujenzi huo tunaomba wawasiliane na Viongozi wetu Mwenyekiti Veronicha Chambuso 0717251441 Makamu Mwenyekiti Noel Kiunsi 0765694533 na Katibu John Kitundu 0754820523,”alisema.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here