Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa Wakala wa vipimo Deogratius Maneno akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Kwenye maonyesho ya tano ya Kitaifa ya Madini yanayofanyika mkoani Geita.
Na: Hughes Dugilo, Geita
Jamii imeshauriwa kununua bidhaa katika mizani iliyofanyiwa uhakiki na wakala wa vipimo Tanzania(WMA) ili kuweza kupata bidhaa zilizo sahihi.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Wakala wa Vipimo Deogratius Maneno wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya madini yanayoendelea mkoani Geita.
Maneno amesema kuwa ili kuondokana na changamoto ya uchakachuaji wa mzani ni jukumu la kila mnunuzi kuchunguza mzani huo kama una stika ya Wakala wa Vipimo.
“Kwa sasa Wakala wa Vipimo tumejitahidi kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto za wananchi ikiwa ni pamoja na suala zima la uchakachuaji wa mzani ila kwa sasa tumeboresha kwakuwa ni jukumu letu kuhakikisha mlaji anapata bidhaa sahihi.,”
Amesema lengo la kushiriki katika maonyesho hayo ni kutoa elimu kwa wananchi lakini pia kuhakikisha usahihi wa mzani inayotumika kwa wauzaji na wanunuzi wa madini.
Amesema katika mkoa wa Geita kuna masoko nane ya madini na Wakala wa Vipimo inafanya uhakiki wa mizani yote inayotumika ili iweze kipima kwa usahihi na kuhakikisha biashara zinafanyika kwa haki bila kupunjika kwa upande wowote.
Aidha ameishukuru serikali kwa kiasi kikubwa kwa kuwawezesha kuweza kununua mizani ya kisasa na vifaa maalum vya kuweza kuhakiki mzani ya madini. Pamoja na hayo pia Wakala imewezeshwa mtambo wa kisasa wa kupima dura za maji pamoja na Mita za umeme ili kuendelea kusimamia usahihi wa Vipimo kwenye sekta izo.
Hata hivyo amewataka wachimbaji wadogo wa madini kuhakikisha wanatumia mzani sahihi iliyo hakikiwa na wasishindwe kutoa taarifa pale wanapogundua hitilafu ama udanganyifu wa aina yoyote.
“Sisi Wakala wa Vipimo tuna ofisi katika mikoa yote Tanzania Bara endapo mwananchi unapata changamoto za Vipimo usisite kutembelea ofisi zetu ama kuwasiliana nasi kupitia mitandao yetu ya kijamii ama kwa namba bila malipo 0800110097,”amesema Maneno.
Amesema baada ya maonyesho hayo Wakala wa Vipimo wanatarajia kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo ili kuwajengea uelewa namna ya kufungasha bidhaa zao kwa kutumia Vipimo sahihi ili waweze kuongea thamani kwenye bidhaa zao ili waweze kupata soko la uhakika katika uuzaji wa bidhaa zao.