Home BUSINESS RAIS SAMIA AMPONGEZA DKT. BITEKO KUISIMAMIA SEKTA YA MADINI 

RAIS SAMIA AMPONGEZA DKT. BITEKO KUISIMAMIA SEKTA YA MADINI 

*Ampa Kongole kwa kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa*

Na: Steven Nyamiti, GEITA 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko katika kuisimamia Sekta ya Madini.

Rais Samia amempongeza Dkt. Biteko leo Oktoba 16, 2022 wakati akiwasalimu wananchi wa Runzewe Jimbo la Bukombe mkoani Geita na kuzungumza nao masuala mbalimbali akiwa safarini kuelekea mkoani Kigoma.

“Ndio maana mnaona nawagusa wote nawabadilisha lakini Biteko yupo hapo katika Wizara ya Madini kwa sababu ninaye kijana anayefanya kazi nzuri na anaisaidia Tanzania,” amesema Rais Samia.

Amesema, mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 4 na sasa unachangia karibu asilimia 8 ya mchango wake kwa Taifa.

Vile vile, amemtaka kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini unafikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 ili iweze kuchangia zaidi katika Pato la Taifa.

Aidha, amemtaka kuongeza bidii katika kusimamia shughuli za kuisimamia Sekta kwa kuwa anao uwezo wa kutosha katika shughuli za madini.

Rais Samia amefanya ziara ya siku mbili katika Mkoa wa Geita ambapo amezindua Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu kilichopo mkoani humo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here