Home BUSINESS PROF. MDOE: SEKTA YA UTALII ITAZIDI KUIMARIKA BAADA YA MKUTANO WA KIMATAIFA...

PROF. MDOE: SEKTA YA UTALII ITAZIDI KUIMARIKA BAADA YA MKUTANO WA KIMATAIFA WA (LIATH-DC)

Naibu Katibu Mkuu  wa Wizara ya Elimu, Sayansi  na Teknolojia Prof. James Mdoe amekitaka Chuo cha Taifa cha Utalii kushirikiana na Wizara ya Elimu katika kutoa mawazo yao kuboresha mitaala katika Sekta ya utalii ili Wizara hiyo iweze kuyafanyia kazi.

Profesa Mdoe ameyasema hayo Oktoba 28,2022 alipokuwa akifunga rasmi mkutano wa Pili wa kuunganisha sekta ya tasnia na wasomi katika sekta ya utalii na ukarimu katika nchi zinazoendelea (LIATH), uliofanyika kwa siku mbili Oktoba 27 na 28, 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa Wizara hiyo iko kwenye mkakati wa kupitia sera ya elimu na mafunzo sambamba na kupitia mitaala yote ili kuweza kuendana  wa wakati.

“Katika suala ya kupitia mitaala hata Chuo hiki ch Taifa cha Utalii kinahusika katika kubadilisha mitaala hivyo ni wito wangu kwao na wadau wote wa utalii washirikiane nasisi kwenye zoezi hili ili kupata mawazo yao ya vitu gani tunaweza kuboresha katika sekta ya utalii” amesema Prof. Mdoe.

Aidha Naibu KatibuMkuu huyo, amekipongeza Chuo hicho kwa kuona upo umuhimu wa kujadiliana na wenzao kutoka mataifa mengine ndani ya Afrika kujadili kwa pamoja kupata mbinu na njia bora ya kuimarisha sekta ya Utalii baada ya janga la UVIKO-19, na kwamba anaamini sekta ya utalii itazidi kuimarika baada ya Mkutano huo.

“Mkutano umemalizika na wameweza kutoka na majawabu ya pamoja namna bora ya kuendeleza Sekta ya utalii, hivyo watawasilisha katika Wizara husika ya Utalii lakini pia Wizara yetu ya Elimu ili tuweze kuona namna ya kuboresha katika upande wa mafunzo” amesema.

Mkutano huo wa siku mbili ulishirikisha nchi zaidi ya tano kutoka Bara la Afrika ukijadili mada mbalimbali zilizolenga kuweka mkakati wa ustahimilivu na urejeshaji wa UVIKO-19 kwa utalii katika nchi zinazoendelea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here