Na: Maiko Luoga Dodoma
Kitengo cha Polisi na Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Dodoma Oktoba 12, 2022 kupitia Warsha ya Makasisi zaidi ya 400 wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika DCT Dodoma, walitoa elimu ya kupinga uhalifu na ukatili wa Kijinsia kwa jamii.
Warsha hiyo ilifanyika katika Chuo cha Bibilia cha Kanisa Anglikana Msalato na kuhudhuriwa na Mhashamu Askofu wa Dayosisi Central Tanganyika DCT na Makamu wa Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania (DEAN) Dickson Chilongani.
Mkaguzi wa Polisi Ivonia Mndenye aliwaomba Makasisi kutumia nyumba za Ibada kuhubiri amani na kusimamia familia zao kufuata maadili mema ili kujiepusha na vitendo vya uhalifu.
Christer Kayombo Mkaguzi wa Polisi na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Dodoma alisema ukatili unaanzia nyumbani ilipo familia, hivyo ni vyema kila mmoja kuhakikisha amani na usalama unaimarishwa nyumbani mwake kama maandiko matakatifu ya Dini yanavyoeleza kuwa nyumba iwe Paradiso na siyo uwanja wa vita.
Kwa upande wake Mhashamu Askofu wa Dayosisi Central Tanganyika DCT na Makamu wa Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania (DEAN) Dickson Chilongani, alisema Kanisa litaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali likiwemo Jeshi la Polisi nchini ili kuhakikisha jamii inakuwa salama.