Home LOCAL MSANDO AWAPA SIKU 2 WAFUGAJI KUONDOKA KWENYE VYANZO VYA MAJI

MSANDO AWAPA SIKU 2 WAFUGAJI KUONDOKA KWENYE VYANZO VYA MAJI

NA: FARIDA MANGUBE, MOROGORO.

Serikali  wilayani Morogoro imetoa siku mbili kwa wafugaji waliovamia na kuharibu vyanzo vya maji vya Bodi ya maji bonde la Wami Ruvu kuondoka wenyewe kwa hiyari kinyume na hapo wataondolewa kwa nguvu ili kulinda vyanzo vya maji ambavyo ni tegemezi kwa zaidi ya watu milioni 11 wa mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es salaam.

Akizungumza kwenye kikao kilichowakutanisha wafugaji, ofisi ya bonde la Wami Ruvu, maliasili na viongozi wa Serikali Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Wakili Albert Msando alisema licha ya malalamiko ya wafugaji juu ya kuwa na sheria zao za vijiji zinazowaruhusu kutumia vivuko kunyweshea maji mifugo yao lakini sheria hizo hazizidi sheria za rasilimali za maji za mwaka 2009 na ya mazingira ya mwaka 2004 ambazo haziruhusu shughuli zozote za kibinadamu kufanyika ndani ya mita 60 ya chanzo cha maji.

Alisema pamoja na masuala ya kibajeti kwa kushirikiana na Bonde la Wami Ruvu wanaangalia namna ya kufanya ili kuchukua hatua za dharula kuokoa mifugo sababu wao kama wilaya hawapo tayari kuona mifugo inakufa jambo ambalo litazua taharuki ambapo watachukua hatua zote muhimu kuhakikisha wanaweza kupata maji kwa ajili ya mifugo lakini sio kwa kupeleka mifugo ndani ya vyanzo vya maji.

Hata hivyo aliwataka wafugaji kuacha kulalamika bali kuona namna ya kutumia fedha zao kuongeza nguvu katika ujenzi wa miundombinu ya malambo pamoja na mabirika ya kunyweshea mifugo.

“mkikamatwa kwa kuingia kwenye vyanzo vya maji mnatozwa faini ambazo wakati mwingine zinafika mpaka shilingi mil. 4 kwa mfugaji mmoja, sasa hapo utakuwa umejenga mabirika mangapi kama una moyo wa kujenga mabirika ya kunyweshea wakati birika moja mpaka linakamilika halizidi shilingi milioni moja ” alihoji Wakili Msando.

Awali Mkurugenzi wa bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu Elibariki Mmassy alisema kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) hali ya mvua imepungua kwa sasa ambapo kulipaswa kuwe na mvua za vuli lakini mvua zinatarajiwa kunyesha wiki ya tatu ya mwisho ya mwezi Desemba jambo ambalo ni hatari na halilingani na kiwango cha maji kilichopo kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Mmassy alifafanua kuwa maji yaliyopo kwenye vyanzo vya maji ni asilimia 40% ya mahitaji yote ambapo mitoni kuna lita 4000 wakati wastani wa matumizi maji ya majumbani ni lita 5800 ambapo bodi iliamua kuanza kukagua vyanzo vyake na kubaini wakulima wanaotumia maji ya mtoni na wenye vibali waliwaambia wasitishe na wasio na vibali tuliwaambia wafuate taratibu na mwisho wa siku tuliwazuia kufanya shughuli zozote mtoni.

Alisema changamoto zote hizo zinasababishwa na mabadiliko ya tabianchi, huku kukiwa na ongezeko la kukithiri ukame ambao pia umethiri shughuli za kilimo na ufugaji, pia kupungua kwa kiasi kikubwa kiwango cha maji kwenye mito mikubwa na kusabisha uharibifu unaofanywa na shughuli za kibinadamu  kwa sasa ikiwemo mto Mgeta na Mngazi ambayo yote kwa pamoja inapeleka maji mto Ruvu.

Mmoja wa wafugaji Timoth Olekoyesa aliiomba Serikali kuwaruhusu kutumia vivuko vilivyotengwa kwenye mito hiyo kwa mujibu wa sheria ndogo za vijiji kunyweshea mifugo ili mifugo yao isife kwa kukosa maji kwa sababu wanaweza kupoteza mifugo mingi kwa wakati mmoja.

Hata hivyo aliiomba Serikali kuweka utaratibu wa kutoa elimu ya ufugaji kama ilivyo kwa wakulima wanayofanya kila mara ili kuwawezesha kujua namna bora ya ufugaji na kuhifadhi vyema mifugo yao kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa chama cha wafugaji Wilaya Elia Madihi aliiomba Serikali kuweka utaratibu mzuri wa kuwaondoa wafugaji na kuachana na kuwaondoa kwa kutumia nguvu huku mifugo ikikamatwa na kuwekwa pamoja hali inayosababisha baadhi ya mifugo kufa.

MWISHO.

Previous articleDAWASA YAENDELEZA MRADI WA KUUNGANISHA MAJI WA HNC-MAGEREZA, BOKO
Next articleWAZIRI MKUU AWASILI KOREA KUSINI KWA ZIARA YA KIKAZI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here