Home BUSINESS MCHANGO WA SEKTA YA MADINI WAZIDI KUIMARIKA: DKT. KIJAJI

MCHANGO WA SEKTA YA MADINI WAZIDI KUIMARIKA: DKT. KIJAJI

*Mchango wa wachimbaji wadogo umekua kutoka 4% hadi 40%*

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) amesema mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kuimarika kutokana na kuongezeka kwa usimamizi wa shughuli mbalimbali za madini ambapo mwaka 2021 ulifikia asilimia 7.2 na ukuaji wake ulifikia asilimia 9.6.

Dkt Kijaji ameyasema hayo wakati akifunga Maonesho ya 5 ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya Bombambili mkoani Geita yenye lengo la kukuza dhana ya kukuza teknolojia ya madini.

Pia, Dkt. Kijaji ameitaka Wizara ya Madini kuendelea kusimamia Sekta ya Madini ambayo ni muhimu kwenye mchango wa ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na watanzania kwa ujumla pamoja na kuongeza Pato la Taifa.

Aidha, Dkt Kijaji amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa nia yake ya dhati ya kuleta mabadiliko chanya kwenye Sekta ya Madini kupitia maelekezo yake anayoyatoa.

Dkt. Kijaji ametoa wito kwa Wizara ya Madini kuendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali ili kupata teknolojia ya uongezaji thamani madini kwa lengo la kuachana na usafirishaji wa madini ghafi.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amempongeza Rais Samia kwa kuitangaza vyema Sekta ya Madini duniani kote na kupelekea wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali nchini ikiwemo Sekta ya Madini inayofungamana na sekta nyingine za kiuchumi zikiwemo Sekta za Ujenzi, Viwanda, Kilimo, Usafirishaji na Mawasiliano.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Biteko amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora na kusimamia mikakati iliyojiwekea ili kuwawezesha wachimbaji wadogo waweze kuchimba kwa faida.

“Kufuatia Serikali kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo, mchango wao katika maduhuli ya Serikali umeongezeka kutoka asilimia 4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 40 mwaka 2022 ya maduhuli yote yatokanayo na Sekta ya Madini,” amesema Dkt Biteko.

Previous articleWAZIRI KIJAJI AIPONGEZA STAMICO KUZALISHA MKAA MBADALA ‘RAFIKI BRIQUETTES’
Next articleBoT HARAKISHENI MCHAKATO WA UNUNUZI WA DHAHABU: DKT. KIJAJI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here