Home LOCAL KOREA YAIPATIA TANZANIA MKOPO WA SHILINGI BILIONI 310

KOREA YAIPATIA TANZANIA MKOPO WA SHILINGI BILIONI 310

Serikali ya Jamhuri ya Korea imeipatia Tanzania mkopo wa gharama nafuu wa shilingi bilioni 310 kwa ajili ya upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na uendelezaji na utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi.

Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo baina ya Serikali ya Tanza na Korea Kusini itakayotolewa kupitia benki ya Exim ya Korea, imefanyika leo (Alhamisi, Oktoba 27, 2022) katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Korea Kusini iliyopo Seoul.

Mkataba wa awamu ya pili ya mradi wa upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa NIDA una thamani ya shilingi bilioni 161 na mkataba wa uendelezaji na utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi ambao una thamani ya shilingi bilioni 149.

Akizungumza wakati wa halfa hiyo ambayo ambayo pia ilishuhudiwa na Waziri Mkuu wa Korea Han Duck-Soo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania na Korea zinajivunia mahusiano yaliyodumu kwa miaka 30 ambayo yamekuwa chachu katika kukuza uchumi wa nchi hizo mbili katika sekta mbalimbali.

“Tunaishukuru sana Korea Kusini kwa kuwa miongoni mwa mataifa yanayoshiriki katika kutatua changamoto za kimaendeleo ikiwemo kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Korea (EDCF)”

Amesema kuwa kupitia mfuko huo, Tanzania imeweza kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo madaraja, barabara, kituo cha kisasa cha kusajili meli cha Zanzibar, njia ya kusafirishia umeme, hospitali ya Mloganzila, mradi wa umwagiliaji uliopo Zanzibar na utoaji huduma wa vitambilisho vya Taifa. “Miradi hii yote imegharimu zaidi ya dola za Kimarekani milioni 733.”

Waziri Mkuu amesema kuwa pamoja na mikopo kupitia mfuko wa EDCF, Tanzania pia imekuwa mnufaika wa mikopo kupitia Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA). “Tunaishukuru sana Jamhuri ya Korea kwa kutambua kuwa Tanzania ni nchi ya kipaumbele.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema misaada ya KOICA kwenye eneo la afya, elimu ya ufundi, ufadhili wa masomo imesaidia sana kuleta nguvu na msukumo katika kuongeza kasi ya maendeleo ndani ya Serikali.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema kuwa mkataba wa awamu ya pili wa mradi wa upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa NIDA utaiwezesha mamlaka hiyo kuongeza uwezo wa kutengeneza vitambulisho vya Taifa pamoja na kutunza takwimu. “Mkopo huu utaisaidia NIDA kujikita katika maeneo ya vijijini na kuongeza kasi ya usajili wa vitambulisho.”

Akiuzungumzia mkataba wa uendelezaji na utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi, Katibu Mkuu huyo amesema kuwa mkataba huo utaiwezesha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa na mfumo mpya wa kidijitali badala ya utunzaji wa kwenye makaratasi.

“Tunaamini utaratibu huu mpya utaleta urahisi na utaondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zinatokana na kutokuwepo kwa mfumo rahisi na mzuri wa uhifadhi wa taarifa.”

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Balozi wa Tanzania Nchini Korea Kusini, Balozi Togolani Mavura, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Aboud Hassan Mwinyi na watendaji wengine wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Previous articleRAIS SAMIA YUPO TAYARI MABADILIKO SHERIA YA HABARI – WAZIRI NDUMBARO
Next articleMWANAFUNZI BORA KIDATO CHA NNE AIBUKA SHULE YA NGUVU MPYA 
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here