Wadau walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia wakiwa katika picha ya pamoja katika viwanja vya Hoteli ya Nazareth Mjini Tabora juzi.
Na: Lucas Raphael,Tabora
WAKAZI wa kata 4 zilizopo katika halmshauri ya manispaa Tabora wanatarajia kunufaika na mradi wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa akinamama na watoto baada ya kuzinduliwa kwa mradi huo unaotekelezwa na Taasisi ya Caritas.
Akizungumza Oktoba,2 Mratibu wa Mradi huo Magreth Kusipa alisema wamelenga kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya kijamii ili yashiriki kikamilifu kupambana na vitendo hivyo.
Alibainisha kuwa elimu hiyo ni muhimu sana kwani itasaidia kurejesha maadili ya jamii yaliyoanza kuporomoka ambapo baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakiozesha watoto wao wa kike katika umri mdogo hivyo kuwakosesha haki zao.
Alifafanua kuwa vitendo hivyo sio tu havikubaliki miongoni mwa jamii bali vimekuwa vikirudisha nyuma maendeleo ya mtoto wa kike hivyo kupelekea washindwe kutimiza ndoto zao hata watakapokuwa wakubwa.
Kusipa aliongeza kuwa mradi huo utakaotekelezwa kwa gharama ya sh mil 52.8 utasaidia jamii kubadili mtizamo hasi, tabia na mazoea ambayo yamekuwa yakipelekea baadhi ya wanaume kutothamini wake zao hivyo kuwanyanyasa.
Aidha mradi huo utasaidia kukomesha mimba na ndoa za utotoni miongoni mwa jamii ambapo wataelimishwa faida na madhara ya vitendo hivyo na hatua zitakazochukuliwa na serikali dhidi ya wale wote wanaoendeleza vitendo hivyo.
Aliongeza kuwa elimu ya mapambano dhidi ya vitendo hivyo itatolewa katika kata zote 4 kupitia mikutano ya hadhara ili kuwafikia wadau mbalimbali, makundi ya kijamii, akinamama na wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari.
Mkurugenzi wa Caritas, Timothy Chombo alieleza kuwa mradi huo ni mkombozi kwa wakazi wa kata hizo kwani waathirika wakubwa ni wake zao na watoto wao wa kike waliochini ya miaka 18.
Aliongeza kuwa vitendo hivyo vimepelekea Mkoa huo kushika nafasi ya 2 kitaifa kwa kuwa na asilimia 58 ya matukio ya namna hiyo, hivyo akaomba jamii kuunga mkono juhudi za Caritas ili kukomesha vitendo hivyo.
Naye Mwakilishi wa Baba Askofu Paul Ruzoka wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Tabora, Padre Nicholous Bulabuza aliasa jamii kuendelea kuheshimiana, kupendana na kusaidiana na sio kunyanyasana, Mungu hapendezwi na tabia hizo.
Mradi huo unaofadhiliwa na Taasisi ya Foundation For Civil Society (FCS) utatekelezwa katika kata 4 za Ng’ambo, Kiloleni, Mwinyi na Isevya ambazo ni miongoni mwa maeneo yenye matukio mengi ya ukatili wa kijinsia
Mwisho.