Na: WAF – TANGA.
MGANGA Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amewataka Wataalamu kufanya kazi kwa kujituma na kufuata kanuni na miongozo wakati wa kutoa huduma za afya, ili kuongeza ufanisi na tija katika utendaji wao.
Dkt. Sichalwe amesema hayo wakati akiongea na Wataalamu wa afya ngazi ya Mkoa na Halmashauri ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha huduma za afya nchini, kuelekea Bima ya Afya kwa wote.
Amesema, matatizo mengi yanayotokea katika maeneo ya kutolea huduma za afya, hususan vifo vinavyotokana na uzazi yanasababishwa na Wataalamu wa afya kutofuata miongozo na taratibu za utoaji huduma kwa mgonjwa.
“Ndugu Wataalamu wenzangu tunaweza kupunguza changamoto kama sio kuondoa kabisa katika maeneo ya kutolea huduma, hasa changamoto ya vifo vya mama na mtoto, kama kweli tutafuata miongozo. “ Amesema Dkt. Sichalwe.
Sambamba na hilo, ameelekeza kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa ili kuibua magonjwa mbalimbali na kuyatafutia suluhu ili kuwakinga wananchi wanaoenda kupata huduma katika vituo vya kutolea huduma.
Aidha, Dkt. Sichalwe amesema, wamiliki wa huduma za afya katika kituo chochote ni wananchi, hivyo kuwaelekeza viongozi wote wa afya ngazi ya Mkoa, Halmashauri mpaka vituo vya kutolea huduma kuwahusisha wananchi na viongozi wao juu ya shughuli zote zinazofanyika katika vituo vya kutolea huduma.
Kwa upande mwingine Dkt. Sichalwe ametoa wito kwa viongozi kuwashirikisha Wadau juu ya mipango ya kuboresha utoaji huduma kwa wananchi, huku akisisitiza kuwa Wadau ni wasaidizi wa Serikali kutoa huduma za afya zilizo bora kwa wananchi.
Hata hivyo, Dkt. Sichalwe amewaelekeza Wataalamu wa afya, kujenga tabia ya kufanya tafiti za magonjwa mbalimbali yanayoikumba katika jamii ili kuwasaidia kupata suluhu ya changamoto hizo katika jamii, huku akiwahamasisha kujenga tabia ya kujisomea mara kwa mara ili kuongeza ujuzi juu ya magonjwa na namna ya kukabiliana nayo.
Aidha, amemwelekeza Maafisa Utumishi kushirikiana na viongozi wengine kupitia upya mgawanyo wa Watumishi katika maeneo yao ili kuwagawa kulingana na uhitaji na mzigo wa majukumu katika maeneo hayo, jambo litalosaidia kuongeza ufanisi na tija katika utendaji.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Jonathan Budenu amemshukuru Mganga Mkuu wa Serikali kwa kuandaa simamizi shirikishi katika Mkoa wa Tanga yenye lengo la kubadilishana uelewa ili kuboresha huduma kwa wananchi hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inaelekea kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa wote.
Aliendelea kusisitiza, kwa Wataalamu kuendelea kushirikiana katika maeneo yao ya kutolea huduma ili kuongeza kasi ya utoaji huduma bora na zenye ufanisi hali itayosaidia kupunguza malalamiko kwa wateja yanayoweza kuzuilika.
Mwisho.