Home LOCAL DKT BATILDA AHAMASISHA UTALII HIFADHI YA MTO UGALLA

DKT BATILDA AHAMASISHA UTALII HIFADHI YA MTO UGALLA

MKuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian akiongoza msafara wa watalii wa ndani kuingia katika lango kuu la Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla iliyoko MKoani humo hivi karibuni.  

Na: Lucas Raphael,Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian amewataka wakazi wa Mkoa huo, Mikoa jirani, wadau na taasisi mbalimbali kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla iliyoko Mkoani humo ili kufurahia vivutio vya utalii vilivyopo.

Akiongea na gazeti hili ofisini kwake jana  alisema hifadhi hiyo ni mahali sahihi pa kutembelea kutokana na mandhari nzuri na vivutio lukuki vilivyopo, aliomba jamii na wadau mbalimbali kuchangamkia fursa hiyo ili kujionea vivutio hivyo.

Aliishukuru serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kupandisha hadhi hifadhi hiyo ili kupanua wigo wa utalii na kuufanya Mkoa huo kupiga hatua kubwa kimaendeleo kupitia fursa ya utalii.

Aliwahakikishia wadau kuwa Hifadhi hiyo ni mahali salama kwa watalii wa ndani na nje kwani ulinzi na usalama vimeimarishwa kwa asilimia 100 na doria inafanyika kwa masaa 24 katika maeneo yote.

Dkt Batilda alisisitiza kuwa Msimamizi Mkuu wa Hifadhi hiyo na timu yake wameendelea kufanya maboresho makubwa katika eneo hilo ili kutoa fursa kwa watalii kupata huduma stahiki na bora wanapokuwa katika eneo hilo.

Alifafanua kuwa eneo hilo ni maalumu kwa utalii tu, shughuli nyinginezo za kibinadamu haziruhusiwa na kuonya kuwa yeyote atakayeenda kinyume hawatasita kuchukua hatua kali za kisheria.

Aliwashukuru wakazi wa Mkoa huo wakiwemo Wakuu wa Taasisi na wanahabari kwa kujitokeza kwa wingi kutembelea hifadhi hiyo na kuyataka makundi mengine ya kijamii wakiwemo viongozi wa kisiasa,  watumishi wa kada mbalimbali, wanafunzi, taasisi, mashirika na wananchi wote kuchangamkia fursa hiyo.

‘Hifadhi hii ina mandhari nzuri sana, nimeitembelea na kujionea vivutio vilivyopo,  wanyama wa nchi kavu na majini, ndege na chakula kizuri, hakika ni eneo sahihi kwa utalii, nawakaribisha wote, njooni muone raha ya Mto Ugalla’, alisema.

Msimamizi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi Ole Meikas alieleza kuwa  eneo hilo ni kivutio kizuri sana kwa watalii kutokana na vivutio vilivyopo ikiwemo wanyama, ndege na vinginevyo.

Alitaja baadhi ya vivutio vilivyopo kuwa ni wanyama na ndege wa aina mbalimbali wakiwemo tembo, simba, pundamilia, nyati, twiga, nyumbu, viboko, mamba, swala na ndege zaidi ya aina 57.

Alisisitiza kuwa Hifadhi hiyo fursa muhimu sana kwa uchumi wa wakazi wa wilaya ya Kaliua, Mkoa na taifa kwa ujumla kutokana na fursa lukuki zilizopo.

Naye Mkuu wa wilaya ya Kaliua, Paul Chacha alieleza kuwa Hifadhi hiyo ni urithi wa wananchi wa wilaya hiyo na Mkoa mzima wa Tabora, hivyo wana kila sababu kujivunia eneo hilo, kulitembelea na kushirikiana na Mhifadhi Mkuu kulilinda.

Aliwataka wanaoishi kando kando ya hifadhi hiyo kutoingia ndani ya hifadhi kwa ajili ya kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo uvuvi, kilimo na ufugaji nyuki ili kulinda uoto wa asili wa eneo hilo.

Mwisho.

Previous articleYANGA YAKANUSHA TAARIFA ZA KUONDOKA KWA NABI
Next articleKATA 4 KUNUFAIKA NA MRADI WA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here