Ofisa Mawasiliano na Kampeni wa Shirika la WaterAid na Neema Kimaro(kushoto) akikabidhi msaada wa Katoni za sabuni kwa Ofisa Afya Mkoa wa Dar es Salaam Enezael Ayo leo Oktoba 11 mwaka 2022
Ofisa Afya Mkoa wa Dar es Salaam Enezael Ayo akiwa (wa kwanza kulia) akiwa mikono kwenye moja ya eneo ambalo limejengwa na Shirika la WaterAid katika Ofisi za mkoa huo ikiwa ni uhamasishaji wa Unawaji Mikono kwa wakazi wa Dar es Salaam.
Moja ya kituo cha kunawa mikono kilichojengwa na Shirika la WaterAid katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala ambacho kinatumiwa na wananchi kunawa mikono
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwananyamala Dk.Aileen Barongo( kushoto) akipokea sehemu ya Katoni za sabuni kutoka kwa Ofisa Mawasiliano na Kampeni wa Shirika la WaterAid Tanzania Neema Kimaro ( kulia)
Ofisa Mawasiliano na Kampeni wa Shirika la WaterAid Tanzania Neema Kimaro akinawa mikono kwa maji tiririka na sabani katika kituo maalum Cha kunawa mikono kilichojengwa na Shirika lao katika Ofisi za Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kukabidhi msaada wa Katoni 11 za sabuni.
Ofisa Muuguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala Upendo Nkurumah ( wa kwanza kulia) akiwa na Kaimu Mganga Mkuu katika hospitali hiyo Dk.Aileen Barongo wakionesha kwa vitendo namna sahihi ya Unawaji mikono baada ya kupokea msaada wa Katoni za sabuni kutoka Shirika la WaterAid Tanzania leo Oktoba 11, 2022.
Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye eneo Maalum la kunawa mikono katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala
Kaimu Mganga Mkuu katika hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwananyamala Dk Aileen Barongo( wa pili kushoto) akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea msaada wa Katoni za sabuni kutoka kwa Ofisa Mawasiliano na Kampeni wa Shirika la WaterAid Tanzania Neema Kimaro ( hayuko pichani).
Na: Said Mwishehe, Michuzi TV.
WANANCHI wa Mkoa wa Dar es Salaam wameshauriwa kujenga utamaduni wa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabani kama hatua mojawapo ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza hasa kipindi hiki ambacho nchi jirani ya Uganda kuna tishio la ugonjwa wa Ebola.
Ushauri huo umetolewa leo Oktoba 11,2022 na Ofisa Afya Mkoa wa Dar es Salaam Enezael Ayo alipokuwa akipokea msaada wa katoni 11 za sabuni ambazo ni sawa na lita 220 zilizotolewa na Shirika la WaterAid Tanzania kwa lengo la kukabiliana na tishio la Ebola.
Ayo amesema pia msaada huo umekuja wakati muafaka kwani Oktoba 15 ya wiki hii tunaadhimisha Siku ya Unawaji Mikono Duniani.Katika kuadhimisha Siku hiyo wamekuwa wakishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo WaterAid ambao wamekuwa wakifadhili siku ya Unawaji mikono.
“Wakati tunaelekea Oktoba 15 ambayo ni Siku ya kuadhimisha unawaji mikono duniani niendelee kutoa mwito kwa wadau wengine waendelee kuisaidia jamii kwenye unawaji mikono kwasaabbu jamii inahitaji kunawa mikono,”amesema.
Amesema wanafahamu wametoka kwenye janga la COVID-19 lakini sasa kuna tishio la Ebola ambalo lipo nchini Uganda na kama inavyoeleka nchi hiyo iko jirani na Dar es Salaam ambayo ni kitovu cha biashara,hivyo kuna ndege nyingi zinaingia kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Uganda.
“Kwa hiyo wananchi wote tunatakiwa kuwa na usafi wa mikono na tunaponawa mikono sio tu inazudia COVID- 19 bali inazuia na magonjwa mengine ya kuhara, kipindupindu na magonjwa mengine.Kauli mbiu ya katika maadhimisho ya mwaka huu inasema mikono salama kwa kila mmoja.
“Kwa hiyo tuungane kuhakikisha kila mmoja anakuwa na mikono safi ili kuepusha kupata magonjwa au kuambukiza magonjwa kwa wengine , kwa hiyo kuelekea siku hii ya unawaji mikono Mkoa wa Dar es Salaam tumehakikisha kila kituo cha afya ,kila zahanati, kila taasisi kunakuwa na maeneo ya kunawa mikono kwa ajili ya kujikinga na maradhi,”ameongeza.
Kuhusu msaada wa WaterAid , amesema baada ya kumpokea msaada huo wa sabuni watagawa katika Hospitali ya Mwananyamala pamoja na kwenye vituo vya afya vidogo na zahanati na wataangalia kwenye uhitaji mkubwa.
Akizungumzia muamko wa wa Unawaji Mikono amesema wakati wa janga la Corona muamko ulikuwa mkubwa lakini hivi Sasa muamko umepungua lakini Mkoa wa Dar es Salaam umeendelea kuweka mikakati kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kunawa mikono wakati wote.
Kwa upande wake Ofisa Mawasiliano na Kampeni wa Shirika la WaterAid Tanzania Neema Kimaro amesema msaada wa sabuni ambazo wamezotoa kwa Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam na Hospitali ya Mwananyamala unalenga kusaidia kukabiliana na Ebola.
“Tumekabidhi katoni 11 za sabuni ambazo ni sawa na lita 220 kwa ajili ya kusaidia kuzuia maambukizi ya Ebola, kama tunavyofahamu nchi jirani ya Uganda inakabiliwa na tishio la Ebola ,hivyo tumeamua kukabidhi msaada huu na kama mnavyoona vituo vya kunawawia mikono tumevitengeneza sehemu mbalimbali hapa Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar.
“Tulivijenga wakati wa kukabiliana na janga la COVID-19 ambalo halijaisha na katika kuchukua tahadhari ya Ebola tumeona ni vizuri tukaja kukabidhi sabuni na tunaamini wadau wengine kwenye masula ya unawaji mikono wataungana na sisi kuelekea maadhimisho ya Siku ya unawaji mikono duniani Oktoba 15,”amesema .
Aidha amesema kwa sasa unawaji mikono umekuwa chini lakini wanafahamu kubadilisha tabia sio jambo la siku moja bali linachukua muda mrefu mtu kuona unawaji mikono ni jambo la kila siku.“Hivyo tusichoke kunawa mikono mikono ni kwa ajili ya faida ya kwetu sote.”
Wakati huo huo Kaimu Mganga Mkuu Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwananyamala Dk.Aileen Barongo alisema wanashukuru kwa msaada ambao wameupata kutoka Shirika la WaterAid na kwamba wao wanaendelea kuhamasisha watu kunawa mikono.
“Kwa hospitali ya Mwananyamala watu wanaofika hapo wamekuwa wakinawa mikono na kuna vituo vya kutosha watu kunawa mikono.Hata hivyo tunaendelea kuhamasisha watu kujenga utamaduni wa kunawa mikono kwa hiyari badala ya kushurutishwa,” amesema na kuongeza wanatoa shukrani kwa WaterAid kushirikiana nao kuhakikisha wananchi wanaendelea kunawa mikono.