Home LOCAL WIKI YA VIZIWI KITAIFA KUFANYIKA MTWARA

WIKI YA VIZIWI KITAIFA KUFANYIKA MTWARA

Na: Heri Shaaban

MADHIMISHO ya Wiki ya Viziwi Kitaifa kwa mwaka huu yanatarajia kufanyika mkoani Mtwara.

Kwa hapa nchini maadhimisho hayo yalianza kuadhimishwa mwaka 2012 na hadi sasa yameweza kufikia mikoa tisa.

Hayo yalisemwa na Mratibu wa Masuala ya Jinsia kutoka Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Lupi Mwaisaka, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana.

Alisema kila mwaka wiki ya tatu ya mwezi Septemba ni ya madhimisho ya wiki ya viziwi Duniani na kwamba lengo la madhimisho hayo ni kutoa mwamko kwa jamii kuhusu masuala mbalimbali ya viziwi.

“Madhimisho ya kitaifa wiki ya viziwi mwaka huu tunatarajia kufanya mkoani Mwara, serikali na wadau wa maendeleo inatambua mahitaji ya viziwi kwenye nyanja mbalimbali na kuchukua hatua kuwajumuisha Ili kuondoa unyanyapa,” alisema Lupi.

Lupi alisema maadhimisho hayo yatakayoanza Septemba 25 mpaka Oktoba Mosi yanaongozwa na kaulimbiu inayosema “Kujenga Jamii Jumuishi”.

Aidha alisema wanatarajia mawaziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa, watahudhuria.

Katika hatua nyingine Lupi alisema CHAVITA kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), linaendesha kampeni ya uhamasishaji wa elimu sahihi juu ya chanjo ya UVIKO -19 kwa jamii ya viziwi kwenye mikoa mitatu ya Arusha, Mwanza na Mbeya.

Alisema elimu hiyo imewawezesha viziwi kuamua kwa hiari yao kupata chanjo chini ya wataalam wa afya.

Alisema hadi sasa mradi umeweza kuwafikia wananchi 42,961 ambapo wameweza kuongeza idadi ya waliochanjwa kutoka 87 hadi kufikia 303 ambao ni ongezeko la viziwi 216.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here