Home LOCAL SERIKALI ITAENDELEA KUCHUKUA HATUA MADHUBUTI KUHAKIKISHA NHIF INAZIDI KUIMARIKA: UMMY MWALIMU

SERIKALI ITAENDELEA KUCHUKUA HATUA MADHUBUTI KUHAKIKISHA NHIF INAZIDI KUIMARIKA: UMMY MWALIMU

DODOMA.

Serikali imesema kuwa kuna hatari ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuelemewa na gharama za matibabu kutokana na kuongezeka kwa idadi  kubwa ya wanufaika wenye magonjwa yasiyoambukizwa ambayo gharama zake za matibabu huwa  kubwa.

Hayo yameelezwa Leo Septemba 1,2022  Jijini Dodoma na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akitoa taarifa ya hali ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambapo amesema kama Serikali haitochukua hatua stahiki za kudhibiti magonjwa hayo basi mfuko huo utaelemewa na gharama za matibabu.

Amesema kulingana na takwimu zilizopo, gharama za magonjwa yasiyo ya kuambukizwa zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 35.65 mwaka 2016/17 hadi shilingi bilioni 99.09 mwaka 2021/22.

“Gharama za kuhudumia wagonjwa wa saratani wanaopata tiba za mionzi na chemotherapia (chemotherapy services), kupitia Mfuko ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 9 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 22.5 mwaka 2021/22.” Alisema Waziri Ummy.

Kwa upande wa huduma za matibabu ya figo kwa wanachama wanaopata huduma ya kuchuja damu (hemodialysis services), gharama ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 9.5 mwaka 2015/16 kufikia shilingi bilioni 35.44 mwaka 2021/22, huku idadi ya wagonjwa wa figo ikiongezeka kutoka 280 mwaka 2014/15 hadi kufikia 2,099 mwaka 2021/22.

Gharama za matibabu ya moyo kwa wanachama wa Mfuko wanaopata matibabu ya upasuaji wa moyo (minimal and invasive cardiac procedures), ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 0.5 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 4.33 mwaka 2021/22 ambapo gharama za vipimo vya CT scan na MRI zikiongezeka kutoka shilingi bilioni 5.43 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 10.87 mwaka 2021/22.

“Kwa muelekeo wa takwimu hizi, ni wazi kuwa kama hatutachukua hatua madhubuti kama nchi, kuna uwezekano wa Mfuko kwa siku za mbeleni kushindwa kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.” Alisema

Aidha amesema Serikali itaendelea kubuni mikakati ya kukinga magonjwa hayo pamoja na kupambana nayo kadri yanavyojitokeza.

Amesemea pamoja na uwepo wa ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambukiza, pia sababu nyingine inayohatarisha uhai na uendelevu wa Mfuko huu ni vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watoa huduma na wanachama wa Mfuko, vitendo hivi vinalenga kujipatia manufaa kinyume na utaratibu.

Ambapo katika mwaka wa fedha 2021na 22 jumla ya wataalum 65 wamefikishwa katika mabaraza yao ya kimaadili kutokana na kukiuka taratibu na miongozo ya taaluma za Afya.

Aidha amewatoa wasiwasi wadau wa NHIF wakiwemo wanachama, watoa huduma pamoja na watanzania wote kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa Mfuko huo unakuwa imara, endelevu na stahimilivu kwani kwa sasa, ni moja kati ya mfumo unaotumika katika kuhakikisha huduma za afya zinatolewa nchini.

“Mfuko huu ndio umekuwa tegemeo la watanzania wengi hususani wa kipato cha chini. Na Mfuko huu pia ndio umekuwa tegemeo la vituo vya kutoa huduma za Afya nchini. Pamoja na kuwa na wanachama asilimia nane (8) tu ya Watanzania wote, vituo vingi vya kutolea huduma vinategemea mapato kutoka katika Mfuko kwa zaidi ya asilimia 70.” Alisema waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo itaweka mazingira kwa kila Mtanzania kuwa na Bima ya Afya ili kuwezesha dhana ya kuchangiana gharama za matibabu na hivyo kuwaepusha wananchi katika hatari ya janga la umaskini pindi wakiwa wagonjwa au wanapougua.

“Hatutakubali kuona Mfuko huu unatetereka kwa sababu Changamoto zilizoko tunazifahamu na mikakati ya kuzishughulikia imeanza kutekelezwa” amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here