Home BUSINESS TPA, BANDARI YA ANTWERP KUONGEZA USHIRIKIANO

TPA, BANDARI YA ANTWERP KUONGEZA USHIRIKIANO

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na Bandari Antwerp ya Ubelgiji zimeahidi kuongeza ushirikiano ili kuongeza ufanisi katika shughuli za bandari pamoja na Chuo cha Bandari nchini.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Juma Kijavara amebainisha hayo wakati alipokutana kwa mazungumzo na Uongozi wa Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bandari hiyo Bw. Kristof Waterschoot katika Ofisi za Mamlaka hiyo Jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia ugeni huo, Mhandisi Kijavara amesema umetembelea bandari hiyo kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina yao na kuona maeneo gani wanaweza kuanzisha ushirikiano na kukuza ufanisi wa huduma za bandari.

“Tumeona tushirikiane na wenzetu walioendelea zaidi katika bandari ili kuboresha ufanisi katika bandari zetu na maeneo tunayoona ni ya kipaumbele ni ushirikiano katika kuboresha Chuo chetu cha bandari, kuimarisha shughuli za bandari za kila siku, miundimbinu na masuala ya Tehama,”amesema Kijavara.

Pamoja na mambo mengine, Kijavara amesema kwa mwaka wa kalenda 2021 walihudumia meli 50 – 60 kwa mwezi lakini kutokana na kuongezeka kwa ufanisi, TPA inahudumia meli kati ya 65 – 80 kwa mwezi na kuchangia makusanyo kuongezeka kutoka Sh bilioni 70 – 75 kwa mwezi hadi kufikia Sh bilioni 90 – 100 kwa mwezi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji, Bw. Kristof Waterschoot amesema kuwa lengo la ziara yake nchini ni kuangalia maeneo ya ushirikiano baina ya Bandari ya Antwerp na Mamlaka ya Bandari ya Tanzania ili kuboresha zaidi ufanisi wa bandari pamoja na Chuo cha Bandari ili kuweza kuwajengea uwezo zaidi wanafunzi wanaosoma na watakaosoma katika chou cha bandari.

“Tunaamini ushirikiano baina ya Bandari ya Antwerp na TPA utaimarisha sekta ya bandari zetu na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za bandari kwa maslahi ya mataifa yetu,” amesema Bw. Waterschoot.

Uongozi wa Bandari ya Antwerp ya Ubelgiji umewasili nchini leo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo mbali na kuitembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), pia ujumbe huo utafanya ziara katika Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) pamoja na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Jijini Dodoma.

Previous article‘SCHOLAR JUNIOR PATROL’ MPANGO UNAONUSURU WANAFUNZI WANAOTUMIA BARABARA
Next articleMWAKIBETE ATOA WITO UTUNZAJI WA MAZINGIRA KATIKA USAFIRI WA MAJI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here