Home BUSINESS TIC YATEMBRLEA KIWANDA CHA KUTENGENEZA VIOO MKURANGA

TIC YATEMBRLEA KIWANDA CHA KUTENGENEZA VIOO MKURANGA

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimetembelea mradi unaosimamiwa na Sapphire Float Glass (Tanzania) Company Limited uliopo Mkuranga mkoani Pwani leo tarehe 02 Septemba, 2022.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Ndugu John M. Mnali amesema kama Kituo kazi kubwa wanayoifanya ni kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini lakini pia kuwasaidia wawekezaji kupata vibali na leseni mbalimbali ili waweze kufanya uwekezaji.
“TIC hatuishii hapo, tunawatembelea wawekezaji kujua changamoto zozote wanazokuwa nazo wakati wa utekelezaji wa miradi yao ili kama kuna changamoto zozote waweze kusaidiwa miradi yao isikwame iweze kuendelea” amesema Ndg. Mnali.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji ameongeza kuwa kiwanda hiki cha kutengeneza vioo kwa ajili ya ujenzi wa majengo mbalimbali, kitakuwa ni cha kwanza kwa Tanzania na cha tatu kwa ukanda wa Afrika cha kwanza kikiwa nchini Naijeria na cha pili kipo nchini Afrika Kusini.
“Kiwanda hiki kinatarajia kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 720 na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 700 za vioo kwa siku watakapoanza uzalishaji mwezi wa Aprili, 2023”, amesema Mnali.
Hata hivyo uwekezaji huu ni matokeo ya mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini. Kwakuwa muwekezaji huyu ameanza kuwekeza kwenye kiwanda cha Goodwill ambacho kinatengeneza marumaru(tiles) hapa hapa Mkuranga na kwa sasa hatuagizi marumaru kutoka nje ya nchi na hata kama zinaagizwa ni kwa kiasi kidogo, amesema ndugu Mnali.
Kwa upande wake mwakilishi wa mradi huo Bi. XUEHUA CHEN amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri kwa Wawekezaji na kusema kupitia Kituo Cha Uwekezaji Tanzania(TIC) wamekuwa wakipata mwongozo wa haraka zaidi katika ujenzi wa kiwanda hicho na kusisitiza kuwa ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Machi na kuanza uzalishaji mwezi Aprili mwaka 2023.
Mradi huu unatarajia kutoa ajira zaidi ya 1500 za moja kwa moja kwa Watanzania na kama nchi uwekezaji huu utasaidia kuokoa fedha za kigeni lakini kuongeza mapato kwa kuuza bidhaa hizi nje ya nchi.
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI (TIC)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here