Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na waandishi wa habari kuelezea Mkutano wa wanawake na vijana utakaofunguliwa rasmi kesho na Rais Samia Suluhu hassan Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa sekretarieti ya eneo huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) Mhe. Wamkele Mene (kushoto) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari (hawamo pichani) mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. (kulia) ni Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji.
Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) pamoja na Katibu Mkuu wa sekretarieti ya eneo huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) Mhe. Wamkele Mene (kushoto) wakizungumza mara baada ya katibu huyo kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA: HUGHES DUGILO)
DAR ES SALAAM.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa wanawake na vijana katika Biashara chini ya mkataba wa Eneo huru la Biashara la Afrika utakaofanyika kwa siku tatu Kuanzia Septemba 12 hadi 14 Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 11,2022 Jijini Dar es Salaam alipokuwa akimpokea Katibu Mkuu wa sekretarieti ya eneo huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema mkutano huo unalenga kuwakutanisha pamoja wanawake na vijana katika Biashara kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika biashara.
Amesema kuwa Mkutano huo ni hatua ya kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika biashara na katika mchakato wa kuanzisha Itifaki ya Wanawake na Vijana katika Biashara inayoandaliwa na Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara la Afrika kwa kushirikiana na nchi wanachama wa AfCFTA.
“Mkutano huu utaongozwa na Kauli Mbiu isemayo ‘Wanawake na Vijana: Injini ya ya Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika’ (Women and Youth: The Engine of AfCFTA Trade in Africa) ambayo inafafanua kwa usahihi jukumu kuu la wanawake katika Afrika na Uchumi wa Dunia na umuhimu wa kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki na kutumia ipasavyo fursa za Biashara katika Eneo Huru la Biashara la Afrika ili kuongeza ajira na kukuza uchumi imara kwa Taifa na Jamii kwa ujumla” amesama Dkt. Kijaji.
Ameeleza kuwa Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki wapatao 500 ambao ni pamoja na Viongozi mbalimbali wanawake katika ngazi ya Marais, Marais Wastaafu, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu, Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Kimataifa, Watu Mashuhuri, Mawaziri wanaosimamia sekta za biashara na Masuala ya Jinsia na Wanawake, Vijana na Wafanyabiashara.
Aidha, Sambamba na mkutano huo, kutakuwa na maonesho ya wafanyabiashara yatakayohusisha wafanyabiashara wanawake na vijana kutoka katika nchi 55 za Afrika.
“Mkutano huu wa Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika, ni mkutano wa kwanza kufanyika tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika. Hivyo, kwa ujumla, mkutano huu utatoka na mapendekezo ya Kisera na Mikakati madhubuti ya kuimarisha uwezo wa Wanawake na Vijana kutumia fursa zinazotokana na Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika”
Mkutano huo utajadili mada mbalimbali muhimu ambazo ni pamoja na:Changamoto wanazokumbana nazo Wanawake na Vijana katika biashara za Mpakani (Reflecting on Challenges Women and Youth face in Cross Border Trade in Africa);Namna ya kusaidia Wanawake na Vijana ambao ni kichocheo katika Sekta ya Ubunifu Barani Afrika (Supporting Women and Youth as Drivers of the Creative Industry in Africa);Namna ya kutumia nyenzo za Kidigitali za Biashara ili kuimarisha ushindani Wanawake na Vijana katika Soko la Eneo Huru la Afrika la Biashara (Leveraging Digital Solutions to Trade to Enhance Women’s and Youth’s Competitiveness in the AfCFTA Market).
Pia, namna ya kusaidia urasimishaji wa biashara za Wanawake na Vijana ili waweze kunufaika zaidi na Mkataba wa Eneo Huru (Women and Youth in Informal Cross Border Trade: Supporting the formalization of women and youth in trade for greater benefits under the AfCFTA).
Aidha kutakuwepo Majadiliano kuhusu Itifaki ya Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (Youth Roundtable on the AfCFTA Protocol on Women and Youth in Trade); na kuimarisha ushirikishwaji wa Wanawake na Vijana katika masuala ya kifedha (Promoting Financial Inclusion for Women and Youth in Trade).
Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area-AfCFTA) ni eneo Huru la Biashara lenye jumla ya nchi 55 za Afrika zenye jumla ya watu bilioni 1.2 na Pato la Taifa (GDP) la Dola za Kimarekani trilioni 3.4 ambapo Tanzania ni mwanachama.