Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) amepongeza juhudi kubwa zilizofanywa na Viongozi wa Wilaya ya Halmashauri ya Maswa kwa kushirikiana na kituo cha zana za kilimo na teknolojia vijijini (CAMARTEC).
Mhe. Kigahe ameyasema hayo leo tarehe 6. Septemba, 2022 katika ukumbi wa Wizara uliopo mji wa Serikali Mtumba aliposhuhudia utiaji saini wa hati za makubaliano (MoU) baina ya kituo cha zana za kilimo na teknolojia vijijini (CAMARTEC) na Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kuhusu uanzishwaji wa kitovu cha Teknolojia za kihandisi (Engineering Technologies Hub – ETH) katika kijiji cha Mwandete Wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu.
“Juhudi kubwa za rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuinua sekta kilimo kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa ajili ya chakula na malighafi za viwanda vyetu, hivyo tutumie rasilimali za nchi kwa manufaa ya wananchi wetu katika kuwaletea maendeleo” Amesema Mhe. Kigahe.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa kituo cha zana za kilimo na teknolojia vijijini (CAMARTEC) Mhandisi Pythias Ntella ameleza kuwa wafanyabiashara wa Maswa walikuwa wanakutana na changamoto ya ukaushaji wa viazi hasa katika kipindi cha mvua na ukaushaji kuchukua muda mrefu kutokana na ukosefu wa nishati ya jua hali inayosababisha Kiwanda kushindwa kukidhi mahitaji ya wateja na pia hasara kutokana na kupungua kwa ubora wa viazi.
Mhandisi Ntella amesema kuwa ujio wa Kitovu cha Teknolojia za Kihandisi (KITEKI) kitakuwa ni cha kwanza na cha aina yake nchini, ambapo kitatumika kama mfano (pilot) na kutoa uzoefu mkubwa kwa CAMARTEC utakaoiwezesha kuanzisha vitovu vya namna hiyo kwenye Kanda Saba nchini katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge amesema kuwa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imefanya juhudi kubwa mara baada ya ziara ya Naibu Katibu Mkuu Mhe. Dkt. Hashil Abdallah alipofanya ziara ya Kikazi Wilayani Maswa na kutembelea Kijiji cha Mwandete kilichopo Kata ya Sangamwalugesha Mkoani Simiyu.
“Madhumuni ya ziara ya Naibu Katibu Mkuu Mhe. Dkt. Hashil Abdallah yalikuwa ni kuharakisha utekelezaji wa Mradi wa Uanzishwaji wa Kitovu cha Teknolojia za Kihandisi (Engineering Technology Hub-ETH) unaotarajiwa kuanzishwa kwenye Kijiji cha Mwandete, hivyo natoa shukrani za dhati kwa Viongozi wote waliofanya juhudi kubwa za uanzishwaji wa kituo hiki akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Mkurugenzi wa Halmashauri na waheshimiwa madiwani kwa kukubali kwa kauli moja”. Amesema Mhe. Kaminyoge.
Akitoa neno la Shukrani Mbunge wa Maswa Mhe. Stanslaus Nyongo amesema kuwa uanzishwaji wa Kitovu cha Teknolojia za Kihandisi (KITEKI) katika Kijiji cha Mwandete unaenda kutatua changamoto nyingi wanazokumbana nazo wakulima ikiwemo kukosa teknolojia rais ya kukaushia mazao yao, ajira inaenda kuongezeka na kipato kwa wananchi.
Mhe. Nyongo amesema kuwa pongezi nyingi anazitoa kwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwani amewajali wananchi wa Maswa kwa kuwapelekea fedha za maendeleo kwa ajili ya miradi mbalimbali ya Maendeleo.
MWISHO