Home LOCAL KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA YAIPONGEZA TMDA KWA UDHIBITI WA...

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA YAIPONGEZA TMDA KWA UDHIBITI WA UBORA WA DAWA NA VIFAATIBA

Na: Englibert Kayombo – WAF, Arusha.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imepongeza utendaji kazi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) kwa kufanya udhibiti na kusimamia ubora wa bidhaa hizo kabla ya kufika kwa matumizi kwa wananchi.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Stanslaus Nyongo mara baada ya Kamati hiyo kutembelea Ofisi za Mamlaka hiyo Kanda ya Kaskazini Arusha.

“Leo tumetembelea TMDA kuangalia kazi inazozifanya, tumeona kazi wanazofanya na tumefika hadi hapa katika mpaka wa Tanzania na Kenya, tumejiridhisha na tumeona utaratibu uliowekwa katika kudhibiti wa dawa na vifaatiba ambavyo sio salama” amesema Mhe. Nyongo.

Mhe Nyongo amepongeza pia TMDA kuwa na maabara katika mipaka ya nchi na kusema kuwa maabara hizo zinasaidia kuweza kutambua ubora wa bidhaa haraka zaidi hivyo kuondoa usumbufu wa wasafirishaji bidhaa kusubiri kwa muda mrefu kupata huduma.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema hiyo ziara ya kawaida ya Kamati kumetembelea taasisi za Umma kukagua utoaji wa huduma kwa wananchi.

Dkt. Mollel amesema kuwa Serikali imepokea maoni ya Kamati hiyo ya kuongeza wataalam katika ofisi za TMDA katika maeneo ya mipakani ili kuongeza udhibiti wa uborwa wa bidhaa zinazoingia na kutoka nchini.

Aidha Dkt. Mollel amesema kuwa Kamati imekagua huduma za uchunguzi wa afya maeneo ya mipakani na kuendelea kusisitiza Maafisa Afya katika mipaka kufanya uchunguzi wa kina wa afya ili kujilinda dhidi ya magonjwa ya mlipuko.

Awali akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba Bw. Adam Fimbo amesema kuwa bado wapo watu wanaoingiza bidhaa kwa kutumia njia zisizo rasmi hivyo kuhatarisha afya za wananchi.

“Tuna mipaka 15 ambayo tunafanya uchunguzi na kuruhusu bidhaa rasmi kupita changamoto kubwa ni watu kuingiza dawa duni, bandia amabazo hazijasajiliwa na kuziingiza kwenye soko na ndio kazi kubwa ambayo TMDA tunafanya kudhibiti” amesema Bw. Fimbo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here