Home LOCAL DKT. KIJO BISIMBA: ASASI ZA KIRAIA ZINA MCHANGO MKUBWA KATIKA KUHARAKISHA MAENDELEO...

DKT. KIJO BISIMBA: ASASI ZA KIRAIA ZINA MCHANGO MKUBWA KATIKA KUHARAKISHA MAENDELEO NA HUDUMA MUHIMU KWA WANANCHI

Jamii imeaswa kulipa umuhimu na kipaumbele suala la elimu kama nyenzo muhimu katika kuleta mabadiliko mbalimbali katika jamii sambamba na kuwa na fikra mbadala za kuwezesha jamii kubadilika

Hayo yameelezwa Jijini Dar es Salaam Septemba 23, 2022 na aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt. Hellen Kijo Bisimba alipokuwa akiongea katika mdahalo ulioandaliwa na Jukwaa la vijana la Reach out Tanzania ulioangazia mchango wa Asasi za kiraia katika maendeleo nchini uliofanyika katika ukumbi wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Dkt. Kijo Bisimba amesema, asasi za kiraia zina mchango mkubwa katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja na hata kuisaidia serikali katika kuharakisha maendeleo kwa wananchi kwa kutekeleza majukumu ambayo pia yangeweza kufanywa na serikali.

Ameongeza kuwa kuna wakati Serikali haifikii malengo yake kutokana na sababu mbalimbali hivyo Asasi za kiraia huisadia Serikali kutimiza jukumu hilo.

“Kuna wakati serikali haifikii malengo yake kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchache wa rasilimali, kufuatia hilo asasi za kiraia inakuja hapo kwa ajili ya kuziba hilo gap (uwazi) kati ya mahitaji ya raia na serikali inavyopaswa kukidhi mahitaji hayo” alisema Dkt. Hellen,  na kuongeza

“Ingekuwa kwamba Serikali inafanya kila kitu, hata Asasi za kiraia zisingekuwepo, lakini jambo hilo haliwezekani ndio maana asasi za kiraia zipo dunia nzima”

Ameendelea kwa kusema kuwa, kuna Asasi ambazo zinafanya kazi ya kutoa huduma ambazo zinaweza kufanywa na Serikali, ambazo zinajenga hospitali, vituo vya kulelea yatima, shule na vituo vya kutolea msaada wa kisheria na kwamba zote hizo ni huduma za msingi na muhimu kwa wananchi.

Sambamba na hayo Dkt. Kijo Bisimba amewakumbusha wananchi kufahamu umuhimu wa Serikali na malengo yake pindi inapowekwa madarakani kwa kusema kuwa, baadhi ya malengo mahususi ni pamoja na kutatua changamoto za wananchi ikiwemo changamoto ya umasikini, kuwaletea maendeleo na kuhakikisha wananchi wake wanaishi kwa uhuru na furaha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here