Na. Costantine James, Geita.
Mkuu wa wilaya ya Bukombe Said Nkumba amelitaka Jeshi la Polisi Wilayani Bukombe kuhakikisha harusi zote zinazofanyika wilayani humo zinachunguzwa kwa lengo la kubaini harusi zinazohusisha wanafunzi na watakaobainika wahusika Wachukuliwe hatua za kisheria.
Nkumba amesema hayo katika hafla ya ugawaji wa madawati 100 kwa shule mbili Wilayani Bukombe yaliyotolewa na Wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) amesema wahusika watakao bainika kufungisha ndoa wanafunzi watakamatwa pamoja waandaji na waliohudhuria Sherehe hiyo ili kudhibiti vitendo vya wanafunzi wanaokatizwa Shule kwa kuolewa na kuacha kuendelea na masomo Yao.
Nkumba amesema ni kosa kubwa kumuozesha mwanafunzi wa darasa la saba huku ukiwa na matumaini kuwa mwanafunzi huyo atafeli masomo yake hivyo anapaswa kuolewa kwani kufana hivyo nikinyume na sheria.
Amesema wilaya ya Bukombe imeweka mkakati mkubwa wakufatilia harusi zote zinazoanza baada ya wanafunzi wa darasa la saba kuhitimu masomo yao ya shule za msingi ili kudhibiti wanafunzi hao kuolewa pindi wanapomaliza shule.
Amewataka viongozi wote wa dini wilayani Bukombe kutokufungisha ndoa bila kuchunguza ni nani anaefunga ndoa na ana umri gani ili kujilidhisha wanaofunga ndoa sio wanafunzi kwani wakibaini waliofungishwa ndoa ni wanafunzi watawachukulia hatua kali viongozi hao wa dini.
Meneja wa wakala wa huduma za misitu wilaya ya Bukombe Emilia Alex amesema katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha kila mwanafunzi anakaa kwenye dawati awapo darasani wakala wa huduma za misitu wilaya ya Bukombe wameamua kutoa madawati 100 kwa ajiri ya kuwasaidia wanafunzi.
Nao baadhi ya wanafunzi wa shule ya Msingi Lampalahala na Kayenze wamewapongeza wakala wa huduma za misitu Tanzani (TFS) kwa kuwapa madawati hayo kwani yatawasaidia kuatumia katika kujifunza huku yakiondoa changamoto ya ukosefu wa madawati katika shule zao.