DAR ES SALAAM.
Naibu Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara amewakaribisha Wawekezaji kutoka katika nchi za Afrika kuwekeza nchini Tanzania na kuzalisha bidhaa mbalimbali ili kuongeza wigo wa uwekezaji ndani ya nchi za Afirka utakaochangia ukuaji wa uchumi unaokwenda sambamba na ukuaji wa soko la ajira nchini.
Naibu Waziri Kigahe ameyasema hayo Septemba 22, 2022 katika uzinduzi wa maonyesho ya Kimataifa ya Afrika Mashariki yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Diamond jubilee Jijini Dar es Salaam.
“Tunaweza kuona teknolojia nyingi za kisasa ambazo tunaamini na sisi watanzania tukiwa katika mpango wetu wa kuwa na uchumi wa viwanda lazima tuwe nazo hivyo tunawaomba waonyeshaji hawa kutoka nchi mbalimbali kuja kuwekeza katika nchi yetu , kuzalisha bidhaa mbalimbali ambazo sisi kama Tanzania tunatumia fedha nyingi kuziagiza nje kwaajili ya matumizi yetu ya ndani”
Aidha amesema Kigahe amewaomba wafanyabishara hao kutoka nje waweze kushirikiana na watanzania katika kuleta teknolojia kupitia elimu lakini pia bidhaa ambazo ni muhimu sana kwenye maeneo tofauti tofauti hasa kwenye sekta ya Kilimo kwa kuwa Tanzania ni wazalishaji wa mazao mengi yakiwemo ya chakula na biashara na yanauzwa nje kama malighafi na yakiwa hayajaongezwa thamani na hivyo kupoteza ajira nyingi
Naibu Waziri Kigahe amesema ni muda muafaka sasa teknolojia hizo ziwasaidie na watanzania kuzalisha bidhaa zinazotokana na kilimo, chakula na biashara zinazozalishwa hapa Tanzania. Hata hivyo amehamasisha kupata teknolojia za kisasa ambazo hazina athari kwenye mazingira ambazo zitaendana na hali halisi ili kupunguza fedha nyingi zinazokwenda nje.
“Wekezeni pia katika sekta ya usafiri. Tumeona wenzentu wanatengeneza pikipiki zinzotumia umeme, hizi zitasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira lakini pia kupunguza gharama za kuagiza mafuta na upotevu wa fedha za kigeni na kuongeza ajira nchini na zitaongeza kasi ya maendeleo yetu kwasababu bidhaa nyingi zitaongeza thamani nyingi”. Amesema Kigahe.
Kuhusu vifungashio, Kigahe amesema, moja ya changamoto ambazo zipo katika uzalishaji wa bidhaa Tanzania ni vifungashio vilivyobora ambapo kwa baadhi ya makampuni ambayo yanazalisha vifungashio kutoka India ambao wangekuja kuwekeza nchini Tanzania wangeweza kusaidia kuongeza nguvu ya uzalishaji wa vifungashio bora na vilivyo na bei nafuu na kupunguza uagizaji wa vifungashio kutoka nje vinavyoongeza gharama ya mlaji.
Kigahe amesema kwa sasa vifungashio vingi kwa upande wa Afrika Mashariki vinaagizwa Kenya ila kwa nje vinaaagizwa kutoka china na India.