Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu kijaji akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa Bidhaa mbalimbali nchini alipokutana na waandishi hao leo Septemba 15,2022 katika Ofisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Jijini Dar es Salaam.
(PICHA NA: HUGHES DUGILO)
PICHA ZA WAANDISHI WA HABARI WAKIMSIKILIZA MHE. WAZIRI
Na: Hughes Dugilo: DAR ES SALAAM.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu kijaji amebainisha kuwa hakuna uhaba wa chakula Tanzania na kwamba hali ya chakula ni shwari na kuna akiba ya kutosha.
Waziri Kijaji amebainisha hayo leo Septemba 15,2022 mbele ya waandishi wa habari alipokuwa akitoa taarifa ya mwezi juu ya mwenendo wa bei za Bidhaa mbalimbali ikiwa ni utaratibu wa Wizara yake ya kutoa taarifa hiyo kila ifikapo tarehe 15 katika mwezi.
Amesema kuwa kwa sasa bado nchi ina akiba ya kutosha ya chakula na kwamba wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi juu ya suala hilo.
kuhusu kupanda kwa bei kwa baadhi ya bidhaa hususani chakula katika masoko, Waziri Kijaji amesema Serikali ipo kwenye majadiliano na wasambazaji ili kujua nini kinafanyika katika kuhakikisha ufumbuzi unapatikana.
“Naomba kuwahakikishia wananchi wote kuwa tuna akiba ya kutosha ya chakula, hivyo hakuna uhaba wa chakula nchini”
“Nchi yetu ilikosa mvua za kutosha msimu uliopita na kusababisha hali ya mavuno kupungua, lakini akiba iliyopo inajitosheleza”amesema Waziri Kijaji.
Aidha waziri Kijaji ametolea ufafanuzi suala la wafanyabishara wanaolalamikia kuzuiliwa kusafirisha chakula kwenda nchi jirani au wanaoingiza chakula kutoka nje ambapo amesema kuwa Serikali imeshughulikia suala hilo kutengeneza mfumo wa kuwarasimisha wafanyabiashara hao kwa kuomba kibali kutoka Wizara ya Kilimo kupitia mtandao.
“Serikali imeamua kurasimisha mifumo ya kufanya biashara kwa kuondoa uholela wa kila mtu kufanya anavyotaka na kununua mazao kiholela kuliosababisha usumbufu mkubwa”
“Sasa tumeboresha mfumo wa vibali kwa kurasimisha mfumo huo kwa kutoa vibali maalum kwa wauzaji kutoka nje ili kufanya biashara kwa mujibu wa sheria utakaowasidia kuondokana na usumbufu waliokuwa wakiupata hapo awali” amesema Waziri Kijaji.
Katka hatua nyingine ameongeza kwa kuwataka watanzania wote wanaofanya biashara nje kuhakikisha wanaingia mikataba ya kisheria na wale wanaofanyanao biashara ili kuondokana na matatizo yanayoweza kuwaletea madhara yakiwemo kudhurumiwa.
“Naomba kutoa wito kwa watanzania wote wanaofanya biashara kuhakikisha wanakuwa na mikataba ya kisheria ili kuwahakikishia usalama wa biashara zao na kuhepuka kudhurumiwa, sambamba na kuhakikisha wanazalisha bidhaa zenye ubora zinazokidhi viwango vya soko la Kitaifa na Kimataifa”ameongeza.