Na: Englibert Kayombo WAF – Dar Es Salaam.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeishauri Serikali kutoa kipaumbele kwa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii na kuwa Mamlaka inayojitegemea katika kusimamia usalama wa afya za Watanzania.
Ushauri huo unakuja mara baada ya Kamati hiyo kufanya ziara ya kikazi katika Maabara hiyo iliyopo Jijini Dar Es Salaam kuona shughuli za utoaji huduma pamoja na kuangalia uwekezaji uliofanywa na Serikali katika Maabara hiyo.
“Kazi inayofanywa na Maabara ya Taifa ni kazi kubwa, wanafanya kazi ya kulinda afya za wananchi pamoja na usalama wa nchi ni vizuri kwa Maabara hii ikawa na usimamizi wa kwake na kuwa Mamlaka inayojitegema na kuweza kuweza kufanya kazi vizuri na kulinda afya za Watanzania”. amesema Mwenyekiti wa Kamati hiyo mhe. Stanslaus Nyongo.
Mhe. Nyongo aemsema kuwa Dunia imebadilika na hivi sasa kuna magonjwa mengi ya mlipuko yakiwemo UVIKO-19, Homa ya Mgunda, Ebola pamoja na magonjwa mengine mbalimbali na kubainisha kuwa watu wanaweza kutumia magonjwa hayo kuangamiza watu wengine, hivyo maabara hiyo ni muhimu kwa kufanya kuchunguzi kuona usalama wa nchi yetu.
“Kwa kweli Maabara hii wanafanya kazi kubwa sana, tumeona mitambo mikubwa ya kisasa ambayo inafanya kazi kubwa ya kufanya vipimo mbalimbali, na maabara hii inatumika kufanya vipimo vya ugonjwa wa UVIKO-19 pamoja na magonjwa mengine mbalimbali kwa kweli kazi inayofanyika ni nzuri” amesema Mhe Nyongo
Mhe. Nyongo amesema Kamati itatoa mapendekezo yake kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili Maabara hiyo iwe ni Mamlaka inayojitegemea na kuwa na kazi kuhakikisha kwamba kunakuwa na usalama kwenye nchi yetu kwa kuangalia masuala ya kibaiolojia.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Mhe. Godwin Mollel amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Afya kwa kununua vifaatiba, vifaa vya uchunguzi, ujenzi wa miundombinu pamoja na kuajiri watumishi.
Dkt. Mollel amesema maabara hiyo ina uwezo mkubwa wa kutambua vimelea mbalimbali vya magonjwa na kuiwezesha Serikali kuchukua hatua za haraka katika kudhibiti magonjwa mbalimbali.
Dkt. Mollel amesema uwepo wa Maabara hiyo una faida kwa wananchi kwa kuwezesha utambuzi wa haraka wa magonjwa na kusaidia wananchi kupata tiba stahiki kwa haraka zaidi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Maabara hiyo Bw. Medard Beyanga ameishuruku Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa ndani ya Maabara hiyo.
“Sisi Maabara ya Taifa tumeweka nguvu zaidi katika kupima sampuli za milipuko kama vile Homa ya Mgunda, Kimeta, Surua, Mafua Makali pamoja na magonjwa mengine mballimbali ya mlipuko” amesema Beyanga.
Beyanga naye hakusita kuwasilisha ombi la Maabara hiyo kuwa Mamlaka inayojitegemea katika utekelezaji wa majukumu yake na kuiwezesha kufanya kazi za ulinzi wa afya ya jamii kwa kusimamia ubora wa upiomaji nchini, kutengeza sampuli za kupima ubora na kuzisambaza nchini pamoja na kudhibiti vimelea vya magonjwa.