Na: Paul Zahoro, Mwanza RS.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amewataka viongozi na watendaji wa Halmashauri za Wilaya ya Magu na Kwimba kutoa Elimu ya Kanuni bora za kilimo cha pamba kwa wananchi ili kuwa na ushirikishwaji wa wakulima katika maendeleo ya uzalishaji wa zao hilo.
Ameyasema hayo katika nyakati tofauti leo Agosti 05, 2022 alipofika kwenye wilaya hizo kujitambulisha na kutoa dira ya maendeleo katika kuwahudumia wananchi kufuatia kuteuliwa kwake hivi karibuni na Mhe. Rais kuongoza Mkoa huo.
“Napenda kuwapongeza sana Mkurugenzi na timu yako kwa Ukusanyaji wa mapato ya ndani hadi mmevuka malengo yenu lakini pamoja na hilo nawaomba tutilie Mkazo zao la pamba ambalo ndio uchumi wa wananchi na sina wasiwasi maana nimeambiwa kuwa shamba darasa la Mkoa lipo hapa” Mhe. Malima akiwa Magu.
Akizungumza na watumishi wikayani Kwimba, ametoa rai kwa RUWASA na MWAUWASA kuhakikisha wanaguswa na changamoto ya Maji kwa kila eneo ambalo wananchi wanakosa huduma hiyo na amewataka kuitunza miradi ya maji ili iweze kuwahudumia wañanchi kwa muda mrefu.
Katibu Tawala wa Mkoa, Mhe. Balandya Elikana amewataka watumishi kwenye Wilaya hizo kufanya kazi kwa bidii ili kuwapa wananchi huduma stahiki ili kutimiza dhima na kiu ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutaka kuona wananchi wake wanaendelea kiuchumi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Salum Kali amemhakikishia kiongozi huyo ushirikiano wa dhati na amebainisha kuwa viongozi ndani ya wilaya hiyo wana ushirikiano wa dhati ambao umezaa Matunda ya kuongoza kwa Ukusanyaji wa Mapato ya ndani kwa Mkoa wa Mwanza.
“Mhe. Rais samia Suluhu Hassan ametuletea fedha nyingi sana za kutekeleza miradi mingi kwenye kila sekta na tunayo miradi ya kimkakati, tunajengewa hadi shule kubwa ya kisasa kwa Tshs. Bilioni 4 na itakua na uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi elfu moja na ukienda kwenye Afya miradi inaendelea.” Mhe. Kali.
“Halmashauri ya wilaya ya Kwimba ilikasimia kukusanya Tshs Bilioni 2.4 kwa mwaka wa fesha uliopita na hadi kufikia Juni 30, 2022 tumefanikiwa kukusanya Tshs Bilioni 2.9 sawa na 106% na kwa 2022/23 Halmashauri inakusudia kukusanya Tshs Bilioni 3.1 na tunayo mikakati mbalimbali ya kufikia lengo tulilojiwekea na hata kuvuka lengo.” Mhe. Johari Samizi, Mkuu wa Wilaya Kwimba.