Home LOCAL WAZIRI UMMY AFANYA MAZUNGUMZO NA KAIMU MWAKILISHI MKAZI WA WHO TANZANI

WAZIRI UMMY AFANYA MAZUNGUMZO NA KAIMU MWAKILISHI MKAZI WA WHO TANZANI

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo amekutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania Dkt. Zabron Yoti pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF)nchini Bi.Shalini Bahuguna katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo Yao, Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaniai inathamini mchango mkubwa unaotolewa na mashirika hayo ya kimataifa kwenye maendeleo ya Sekta ya Afya nchini.

“Serikali itaendelea kufanya kazi na WHO, UNICEF pamoja na mashirika mengine ya ndani na nje ya nchi kwa manufaa ya ustawi wa Afya za Watanzania” amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amepongeza jitihada zinazofanywa na wadau hao wa Maendeleo katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kutoa rasilimali pamoja na kujikita katika utoaji wa Elimu na Hamasa ya chanjo dhidi ya UVIKO-19.

Katika kikao hicho pia viongozi hao wamejadili kuhusu zoezi La utoaji wa chanjo aina mbalimbali za watoto ikiwemo zoezi la utoaji wa chanjo ya Polio kwa awamu ya tatu linalotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Kwa upande wao wadau hao wa maendeleo wakizungumza, wameipongeza Serikali katika jitihada inazozifanya kuhamasisha na kutoa elimu ya chanjo dhidi ya UVIKO-19.

Dkt Zabron Yoti, Kaimu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hapa nchini ameihakikishia Serikali kwamba WHO itaendela kuwa mshirika wa karibu zaidi na kutoa msaada wa kitaaluma na rasilimali katika kusaidia Serikali kupambana na majanga ya magonjwa mbalimbali.

Bi.Shalini Bahuguna Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) nchini amesema kuwa ameshuhudia wingi wa Wananchi wakihamasika na kujitokeza kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19 huku pia akipongeza Mkakati wa Wizara pamoja na wadau wengine kutumia watu wenye ushawishi ndani ya Jamii kuhamasisha Wananchi kujitokeza kupata chanjo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here