Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya Dkt.Hellen Mohammed akimhudumia Mteja
Chuo kikuu Mzumbe kimewakaribisha Wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, kutembelea banda la Mzumbe kwenye maonesho ya kitaifa ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Akizungumza na Waandishi wa Habari waliofika katika banda la chuo, Afisa Udahili wa chuo hicho Ndaki ya Mbeya Bw.John Jorrojick, amesema kuwa, Chuo kikuu Mzumbe kinatoa huduma mbalimbali kwenye maonesho hayo ya kitaifa ikiwemo ushauri kuhusu kozi zitolewazo na Chuo, udahili wa papo kwa papo,huduma za kijamii ikiwemo ushauri wa kisheria pamoja na Elimu kwa Umma kuhusu ujasiriamali na biashara.
Chuo Kikuu Mzumbe kinayo mabanda mawili katika maonesho hayo, moja linapatikana karibu na jukwaa kuu la zamani na lingine likiwa katika chumba na 11 kwenye jengo la Sekretariet ya Mkoa .
Maonesho hayo yanayotarajiwa kufikia kilele Jumatatu Agost 8,2022 na yatafungwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan. Kauli mbiu ya maonesho hayo inasema “Agenda 10/30 Kilimo ni Biashara, shiriki kuhesabiwa kwa Mipango bora ya kilimo, mifugo na uvuvi.”