Home BUSINESS WAHIFADHI WATAKIWA KUJENGA MAHUSIANO MAZURI NA WANANCHI

WAHIFADHI WATAKIWA KUJENGA MAHUSIANO MAZURI NA WANANCHI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amewataka wahifadhi kujenga mahusiano mazuri na wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao ya kuhifadhi rasilimali za Taifa.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) alipofanya ziara ya kikazi katika Shamba la Miti Buhindu Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza.

“Jengeni mahusiano mazuri na jamii na zinapokuwa na namahitaji ambayo yako ndani ya uwezo wenu msisite kuwasaidia” Mhe. Masanja amesisitiza.

Amesema uwapo wa mahusiano mazuri utasaidia kupunguza changamoto za uchomaji wa mkaa, wizi wa miti, uingizaji mifugo ndani ya hifadhi na majanga ya moto kwenye misitu.

Aidha, amewataka wahifadhi kuweka utaratibu mzuri wa uvunaji wa miti kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo.

“Tengenezeni mazingira rafiki ya utaratibu ulio wazi wa uvunaji miti, kila mtu aingie kwenye ushindani bila kumuonea mtu” Mhe. Masanja ameongeza.

Naye, Meneja wa Shamba la Miti Buhindi Mussa Tinda amesema shamba limekuwa likisaidia jamii katika Nyanja mbalimbali ambapo jumla ya takriban shilingi milioni 150 zimetumika.

“Tumetoa mifuko ya simenti 300 kwa Kata ya Kafunzo,ujenzi wa mabweni na vyumba vya madarasa,uchimbaji wa kisima cha maji katika shule ya sekondari Ilenza, ujenzi wa kituo cha polisi,kuchangia madawati na ujenzi wa vyumba vya madarasa” Bw. Tinda amefafanua.

Pia amesema shamba limeruhusu wananchi kufanya shughuli za kilimo cha muda mfupi katika maeneo yenye ya wazi na yenye miche midogo na kutoa ajira kwa wananchi.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Shirikisho la Viwanda vya Misitu Tanzania, Bw. Fue Kandawala amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuondoa VAT kwenye miti iliyosimama pamoja na kupunguza tozo za halmashauri kutoka asilimia 5 hadi asilimia 3.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here