Home LOCAL TCU YATAKIWA KUONGEZA JITAHADA KATIKA UTHIBITI UBORA VYUO VIKUU

TCU YATAKIWA KUONGEZA JITAHADA KATIKA UTHIBITI UBORA VYUO VIKUU

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuongeza jitihada katika uthibiti wa Ubora wa vyuo vikuu ili kuwaandaa wahitimu kushindana katika soko la ajira.

Akizungumza mjini Morogoro wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya kuandaa Mitaala inayoendana na Soko la Ajira, Mhe. Kipanga alisema kwamba hatua hiyo itawezesha vyuo kufuata taratibu zilizowekwa na kutoa elimu iliyokusudiwa.

Mhe. Kipanga alibainisha kwamba Serikali inalenga kuimarisha ubora wa elimu kwa ngazi zote kuzingatia falsafa ya kujitegemea yenye kuendana na mazingira ya nchi hivyo TCU ina jukumu la kuongeza juhudi katika kuboresha elimu ya juu.

Hata hivyo, Mhe. Kipanga ameipongeza TCU kwa kutoa mafunzo hayo ya mitaala itakayosaidia kuboresha ubora wa elimu ya juu nchini.

“Mitaala inatakiwa iwe inakata kiu na matarajio ya wananchi ya kupata wahitimu wanaoweza kuhimili changamoto za ushindani wa soko la ajira,” alisema Mhe. Kipanga

Mhe. Kipanga alisema mafunzo hayo ya mitaala kwa taasisi za elimu ya juu yameandaliwa wakati muafaka wakati Serikali inaenda kupitia na kuandaa mitaala mipya itakayojikita katika vipaumbele na mahitaji ya taifa.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa alisema kwamba baada ya mafunzo hayo wanataluuma watakuwa na uwezo wa kuandaa mitaala ambayo itawaimarisha wahitimu katika nyanya mbalimbali za ujuzi na maarifa.

Prof. Kihampa amefafanua kwamba mafunzo hayo pia yamehusisha vyuo binafsi ili kutengeneza uelewa wa pamoja kati ya vyuo vya serikali na binafsi kwa sababu vyote vinatoa elimu kwa Watanzania.

Mafunzo hayo ya siku 3 yameudhuriwa na wataalamu wa mitaala zaidi ya 300 kutoka katika vyuo vikuu vya umma pamoja na vile vya binafsi ili kuwajengea uwezo wanataaluma hao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here