Home LOCAL NCHI JIRANI WAALIKWA TANZANIA KUJIFUNZA NAMNA HUDUMA ZA AFYA ZINAVYOTOLEWA

NCHI JIRANI WAALIKWA TANZANIA KUJIFUNZA NAMNA HUDUMA ZA AFYA ZINAVYOTOLEWA

Na. WAF – Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amezitaka nchi Jirani kuendelea kuja nchini kujifunza namna ambavyo huduma za afya za kibingwa na bobezi zilivyoboreshwa nchini zinavyotolewa kwa kutumia mifumo na teknolojia za kisasa.

Naibu Waziri amesema hayo leo wakati alipotembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Afya wa Malawi Dkt. Enock Phale pamoja na ujumbe wake ambao wamewasili nchini kwa ajili ya kuona na kujifunza namna huduma za afya zinavyotolewa katika Hospitali mbalimbali za umma pamoja na binafsi.

Dkt. Mollel amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutoa huduma za kibingwa na bobezi katika ubora wa hali ya juu, hali ambayo inapelekea wananchi wa nchi za Jirani kuja nchini kupata huduma za afya ambazo zinatolewa katika kiwango na ubora wa kimataifa.

“Tanzania inapokea wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za kiafrika takriban 25, hii inamaanisha kuwa nchi yetu sasa imepiga hatua kubwa katika kutoa huduma za kibingwa na bobezi katika kutibu magonjwa mbalimbali. Hatua hii inatokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan”. Amesema Dkt. Mollel.

Aidha, Dkt. Mollel ameongeza kuwa Tanzania imefikia kuwa na asilimia 85 ya wataalam wazawa ambao wanatoa huduma za upasuaji wa kufungua kifua huku asilimia 15 tu ndiyo wanatoka nje ya nchi lakini wakija nchini wanaacha ujuzi wa ziada kwa wataalam wa ndani.

Nae Naibu Waziri wa Afya wa Malawi Dkt. Enock Phale amesema amefika katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuona namna gani wameweza kutoa huduma za magonjwa na upasuaji wa moyo ili wajifunze na kuanzisha huduma hizo Malawi.

“Tumekua tukitumia fedha nyingi kupeleka wagonjwa wanaohitaji upasuaji wa moyo nchini India, lakini tumeona Tanzania huduma hii inatolewa ndiyo maana tumeamua kuja kujifunza na kuona namna gani na sisi tunaweza kuanzisha taasisi kama hii nchini kwetu”. Amesema Naibu Waziri wa Afya wa Malawi.

Dkt. Phale amemshukuru Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwa kuukaribisha ujumbe wake kuja nchini kuona na kujifunza namna huduma za afya zinavyotolewa ikiwemo mifumo inayotumika kutoa huduma hizo.

Naibu Waziri huyo na ujumbe wake mpaka sasa wametembelea Hospitali za Amana, Bugando, Saifee na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here