Home BUSINESS MRADI WA KUONGEZA USHIRIKI WA VIJANA KATIKA KILIMO WAZINDULIWA

MRADI WA KUONGEZA USHIRIKI WA VIJANA KATIKA KILIMO WAZINDULIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizIndua Programu ya Ajira kwa Vijana Kupitia Sekta ya Kilimo kwenye Banda la Benki Kuu ya Tanzania katika Maonyesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Agosti 3, 2022. Kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Anthiony Mavunde, wa pili kushoto ni Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma, Homela. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitazama mche wa mgomba wakati alipotembelea banda la TAHA katika Maonyesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Agosti 3, 2022. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera na kushoto ni Bwana Shamba Kiongozi wa TAHA, Giliard Daniel. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama ng’ombe wa kisasa wakati alipotembelea banda la kampuni ya Highland Estates Limited katika Maonyesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya Agosti 3, 2022. Kulia ni Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua mradi wa Building a Better Tomorrow (BBT) unaolenga kuongeza ushiriki wa vijana katika kilimo kwa kuwapatia mafunzo, maeneo ya mashamba, mitaji na kuwaunganisha na fursa za masoko.

“Vijana wetu fursa ni nyingi nchini kwetu, sekta ya kilimo inabeba fursa zaidi ya asilimia 50, kitendo cha wizara kuzindua mpango mkakati wa vijana kuingia kwenye sekta ya kilimo ni mpango unaolenga kuboresha uchumi wa mto mmoja mmoja kuanzia umri wa vijana.”

Mheshimiwa Majaliwa amezindua mradi huo wa Program ya Ajira kwa Vijana kupitia Sekta ya Kilimo leo (Jumatano, Agosti 3, 2022) katika maonesho ya siku kuu ya wakulima Nane Nane yanayofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.  

Pia, Waziri Mkuu amewataka vijana wachangamkie fursa zilizopo katika mradi huo ikiwa ni pamoja na kujihusisha na kilimo cha mazao mbalimbali ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Akizungumzia kuhusu mitaji, Waziri Mkuu amesema taasisi zote za kifedha zimepewa maelekezo na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali wanaojihusisha na kilimo.

Amesema vijana wasihofu kuingia katika kilimo, waende wakachukue maeneo na waanze kulima kulingana ardhi ya eneo husika. “Maafisa Ugani watawaelekeza kanuni bora za kilimo.”

Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa mradi huo ni matokeo ya maagizo na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia ya kuhakikisha vijana wanapata fursa katika sekta mbalimbali za kiuchumi zikiwemo za madini, kilimo na nishati.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wananchi watumie maonesho hayo kujifunza teknolojia bora za uzalishaji wa bidhaa za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ili waongeze uzalishaji na tija katika mnyororo wa thamani.

Awali, Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alisema programu hiyo itakayowahusisha vijana wa nchi nzima itaanzania na mkoa wa Dodoma na Mbeya kwa ajili ya majaribio na wametenga ekari 69,000.

Alisema maeneo hayo yataandaliwa na kusafishwa na Serikali kabla ya kuwapatia vijana. “Pia vijana watapatiwa pembejeo na kuweka mifumo mizuri ya umwagiliaji, lengo ni kutengeneza ajira zaidi ya milioni tatu.” 

Previous articleTAASISI YA MIFUPA MOI YATOA ELIMU KATIKA MAONESHO YA NANENANE JIJINI MBEYA
Next articleMAGAZETI YA LEO JUMATANO AGOSTI 4-2022
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here