Na: Asteri Muhozya, Greyson Mwase na Tito Mselem- Mirerani.
Kwa mara nyingine ndani ukuta unaozunguka Migodi ya Tanzanite Mirerani, amepatikana bilionea mpya wa madini ya Tanzanite anayefahamika kwa jina la Anselim Kawishe mchimbaji madogo wa madini hayo baada ya kupata Mawe Makubwa ya kipekee ya tanzanite moja likiwa na uzito wa kilogramu 3.74 na jingine likiwa na uzito wa kilogramu 1.48 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.24
Akizungumza kwenye hafla ya ununuzi wa madini hayo iliyofanyika katika eneo la Kituo cha Tanzanite cha Magufuli kilichopo ndani ya ukuta wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara mapema leo Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adolf Ndunguru amesema kuwa jiwe la kwanza lililopatikana lina na uzito wa kilogramu 1.48 thamani ni shilingi milioni 713.7 na jiwe la pili lina uzito wa kilogramu 3.74 na lina thamani shilingi bilioni 1.53.
Amesema kuwa, thamani ya madini hayo imetokana na vigezo vya kijemolojia ambavyo ni rangi, ubora, uzito, umbo pamoja na mwongozo wa bei elekezi ya Serikali.
“Kipande cha kwanza chenye uzito wa kilogramu 1.48 kina rangi ya AB ambayo ni uzuri wa juu na ubora wa AB ambao ni ubora wa juu na kipande cha pili chenye uzito wa kilogramu 3.74 kina rangi ya BC ambayo ni uzuri wa kati na ubora wa BC ambao ni ubora wa kati,”amesema Ndunguru.
Ameongeza kwamba, kutokana na upekee wake, Serikali imeamua kununua madini hayo na kuyahifadhi na kuongeza kwamba, yatatumika kama kivutio cha utalii nchini hivyo kuongeza mapato Serikalini.
Sambamba na kumpongeza mchimbaji Kawishe amewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini kufuata Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake wanapotekeleza shughuli zao za uchimbaji wa madini.
Naye, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko akizungumza katika hafla hiyo amesema tukio hilo la kihistoria ni la tatu baada ya mchimbaji wa madini ya Tanzanite Saniniu Laizer kuweka historia ya kuwa mchimbaji wa kwanza kupata mawe yenye uzito mkubwa kuwahi kutokea katika historia ya uchimbaji wa madini ya Tanzanite.
Pia, ametaja tukio la mchimbaji mwingine wa madini ya ruby, Sendeu Laizer ambaye alichimba madini ya rubi yenye uzito mkubwa wa tani tano za thamani ya shilingi bilioni 1.7.
Tanzanite kutoka kwa mchimbaji Saniniu Lazier zilikuwa na uzito wa kilogramu 9.2 ya thamani ya shilingi bilioni 4.5, kilogramu 5.8 yenye thamani ya shilingi bilioni 3.3 na jiwe la tatu lenye uzito wa kilogramu 6.33 la thamani ya shilingi bilioni 4.846.
Kwa mujibu wa Anselim Kawishe mchimbaji mpya aliyepata mawe hayo makubwa ya Tanzanite, amesema alianza kufanya kazi za uchimbaji mwaka 2004 kwa kufanya shughuli za wachimbaji wengine hadi mwaka 2012 ambapo alianza rasmi shughuli za kuchimba Tanzanite yeye mwenyewe kwa kuwashirikisha wachimbaji wengine hadi mwaka 2022 ambapo amepata mawe hayo mawili yenye uzito mkubwa na thamani kubwa.
Ameongeza kuwa, kabla ya kupata madini hayo yenye uzito huo, tayari alikuwa amepata madini mengine ya tanzanite yenye jumla ya kilogramu zipatazo 20 zenye muundo wa magonga (rough tanzanite).
“Kwangu mimi tukio hili ni la kistoria, siamini kama kazi yangu imefanya umati huu kukusanyika hapa kwa ajili yangu. Yalikuwa ni matarajio yangu kufanya shughuli za uchimbaji wa madini na ndoto hii nilikuwa nayo miaka 10 iliyopita.
“Matarajio yangu ni kuongeza wigo wa uchimbaji, kuongeza ajira zaidi na kupata kipato zaidi,’’ amesema Kawishe.
Kawishe ambaye ni mzaliwa wa Rombo na mkazi wa jijini Dar es Salaam amesema mbali ya uchimbaji, anafanya shughuli nyingine za kilimo.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka ameishukuru Serikali kwa kukubali kuhamisha shughuli zote zinazohusu mnyororo mzima wa biashara ya Tanzanite ambapo tayari imeanza ujenzi wa Kituo cha Mirerani City ambapo shughuli zote zitafanyika katika kituo hicho.
Aidha, ameipongeza kwa kushughulikia changamoto zilizokuwa kero katika eneo hilo la machimbo ya Tanzanite ambapo tayari imeongeza eneo la ukaguzi, sehemu ya kupumzikia, imefanya matengenezo ya barabara katika eneo linalozunguka machimbo hayo pamoja na kuhamisha biashara ya tanzanite kutoka mkoani Arusha kwenda Mirerani.
“Mhe. Waziri pamoja na kushughulikia changamoto hizo, bado tuna ombi kwa serikali la kujengewa kwa kiwango cha lami barabara inayoelekea katika eneo la machimbo na barabara kutoka eneo la Ukuta wa Magufuli kuelekea barabara kuu na tunaiomba serikali iwaunganishe wananchi na huduma ya maji,’’ amesema Ole Sendeka.