Home LOCAL MABADILIKO SHERIA YA HABARI YANUKIA: WAZIRI NAPE

MABADILIKO SHERIA YA HABARI YANUKIA: WAZIRI NAPE

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

NAPE Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amesema, sehemu kubwa ya mapendekezo ya wadau wa habari nchini yamekubaliwa.

Na kwamba, mazungumzo yanaendelea kati ya wadau wa habari na serikali kuhusu vipengele vingine katika safari ya mabadiliko ya sheria ya habari nchini.

Akizungumza na Salim Kikeke, Mtangazaji Kipindi cha BBC Swahili, Dira ya Dunia, jijini Dar es Salaam tarehe 24 Agosti 2022, Nape amesema wanatarajia kukutana na wadau wa habari katika kikao cha pili.

“Kuna mambo wamekubaliana lakini pia kuna mambo hawajakubaliana. Waliokubaliana ni mengi kuliko wasiyokubaliana, tulichopanga tunakwenda kwenye kikao kingine. Maelekezo ya mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) ni kwamba, zungumzeni mpaka muelewane, mkiishaelewana ndio mtapeleka bungeni,” amesema.

Nape amesema, kinachofanyika sasa ni kupitia vipengele vya Sheria ya Habari ya Mwaka 2016, baada ya wadau wa habari kupiga kelele kwamba vinaminya uhuru wa habari.

“Bahati nzuri kinachofanyika ni kurekebisha sheria iliyopo, Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 ambayo baada ya kutungwa, ilipigiwa kelele hapa na pale.

“Baada ya kupigiwa kelele, Rais wa Awamu ya Sita (Samia Suluhu Hassan), akaagiza kwamba tuipitie upya.., baada ya wadau wa habari kuleta mapendekezo yao na sisi serikali kupitia. Nikaagiza kikao cha wataalamu wa serikali na timu ya wanahabari wakae wapitie tena upya maoni yao na maoni ya serikali, wamepitia wameniletea juzi mapendekezo,” amesema Nape.

Ameeleza matumaini yake ya kupeleka baadhi ya mapendekezo ya sheria hizo katika Bunge la Septemba mwaka huu.