NEVILE Meena, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), amesema iwapo mapendekezo ya sheria ya habari yatapita, yataleta matumaini mapya kwenye tasnia ya habari nchini.
Meena ametoa kauli hiyo leo leo tarehe 27 Agosti 2022 wakati akizungumza na Radio Abood (Abood FM), Morogoro.
“Iwapo mapendekezo haya yatapita na kuwa sheria hata kama si yote, yataleta athari kubwa katika tasnia ya habari.“Ni kwa kuwa, sheria ya huduma ya habari ndio mama wa sheria nyingine, hii imeshika pakubwa ndio maana nasema, itarahisisha sheria zingine kubadilishwa,” amesema Meena.
Amesema, ni jambo la kupongeza kwa hatua ambayo serikali imechukua na ilipofika mpaka sasa, kwani yapo ambayo tayari wamekubakiana na wadau wa habari na mengine hawajakubaliana.
“Kama alivyosema mheshimiwa waziri (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) wakati alipozungumza na BBC.
“Alisema yapo ambayo wameishakubaliana na mazungumzo bado yanaendelea. Sisi tunaamini kuwa, kuna athari chanya itatokea kwenye uandishi wa habari,” amesema.
Amesema, wadau wa habari wameanzisha mchakato huo kwa kuwa, wana nia nzuri na tasnia ya habari na kwamba, serikali imeona nia hiyo ndio maana imeingia kwenye mazungumzo.
“Sisi tuna nia nzuri na mjadala huu na ninaamini tutafika pazuri na kuifanya tasnia ya habari kuwa salama kwa wamiliki wa vymbo vya habari na wanahabari wenyewe.