Home LOCAL KILA MTU ATIMIZE WAJIBU WAKE ILI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA- PROF. MAKUBI.

KILA MTU ATIMIZE WAJIBU WAKE ILI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA- PROF. MAKUBI.

Na:WAF-Dom

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi ametoa wito kwa Wataalamu wa afya wote nchini kutimiza wajibu wao katika maeneo yao ya utendaji ili kuboresha huduma kwa wananchi wanaoenda kupata huduma.

Prof. Makubi ametoa wito huo katika kikao na Waganga Wakuu wa Wilaya, Halmashauri na Wafawidhi kilichofanyika kwa njia ya mtandao (zoom), ambapo Wakurugenzi kutoka Idara na vitengo mbalimbali vya Wizara ya Afya walishiriki pia.

“Nitoe wito kwenu, kila mtu atimize wajibu wake katika utendaji ili kuleta matokeo chanya katika Sekta ya Afya, hili liendane na ubunifu na uchapaji kazi ili tuone mabadiliko katika vituo vyenu vya utoaji huduma.”Amesema Prof. Makubi.

Sambamba na hilo Prof. Makubi amesema, Wizara imejipanga kusimamia utekelezaji wa mwongozo wa ‘clinical audit’ katika ngazi ya utoaji huduma kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya, ili kuboresha huduma na kuleta matokeo kwa wananchi.

Aidha, Prof. Makubi, amewataka Wataalamu wa afya kufuata misingi, miongozo na taaluma zao wakati wa utoaji huduma ikiwemo matumizi ya lugha kwa wateja wanaofika kupata huduma jambo litalosaidia kuondoa malalamiko kwa wananchi yanayoweza kuzuilika.

“Hakuna kitu kinachotia hasira kama vitu vidogo vidogo kushindwa kufanyika katika maeneo ya kutolea huduma, mfano suala la lugha mbaya kwa wananchi wanapoenda kupata huduma, hii ni lazima muifanyie kazi.” Amesema.

Pia, Prof. Makubi amewataka Wataalamu hao kusimamia huduma za mama na mtoto katika maeneo yao ili kuondoa changamoto zinazoweza kuzuilika ikiwemo kuondoa vifo vya mama wajawazito vinavyoweza kuzuilika.

Kwa upande mwingine, amewaagiza kusimamia vizuri fedha za Wadau na za Serikali zinazopelekwa katika vituo vyao ili zilete tija ya kuwahudumia wananchi katika maeneo ya mbalimbali nchini.

Naye, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia masuala ya Afya OR-TAMISEMI Dkt. Grace Magembe amesema katika bajeti ya TAMISEMI 2022/2023 imeweka kipaumbele kikubwa kwenye vifaa tiba, kwenye suala la utumishi, kujenga na kukarabati hospitali mpya za Wilaya na Zahanati lengo ni kuboresha huduma kwa wananchi.

Dkt. Magembe amesisitiza pia ushirikiano katika utendaji kazi kwani lengo ni kuboresha utoaji huduma kwa wananchi, hasa katika wakati wa mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko, huku akisisitiza ushirikiano na Sekta nyingine katika kuboresha Sekta ya Afya.

Hata hivyo, Dkt. Magembe amewashukuru Wataalamu wote kwa kuendelea kujitoa katika kuwahudumia wananchi, huku akiwatia moyo kuendelea kujitoa katika utendaji wao.

Mwisho.

Previous articleBENKI YA NBC, KOLA PRODUCTS WATOA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI KWA VIJANA WA DON BOSCO
Next articleWATOTO WOTE WAPEWE CHANJO YA POLIO, WAPOTOSHAJI TUTAWACHUKULIA HATUA: DC MBONEKO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here