Home LOCAL KAMATI YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII YAISHAURI SERIKALI KUBORESHA...

KAMATI YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII YAISHAURI SERIKALI KUBORESHA UPATIKANAJI WA DAWA NA BIDHAA MUHIMU ZA AFYA

Na: Englibert Kayombo – WAF, Bungeni – Dodoma.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeishauri Serikali kuboresha hali ya upatikanaji wa dawa nchini na kuhakikisha bidhaa muhimu zinapatikana kwa urahisi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Kamati hiyo inayoongozwa na Mheshimiwa Stanslaus Nyongo (Mbunge) kwenye kikao kilichoikutanisha Kamati hiyo, Viongozi na Watendaji wa Wizara Pamoja na Bohari ya Dawa (MSD) katika kumbi za mikutano ya Bunge Jijini Dodoma.

“Kilio cha wananchi ni ukosefu wa dawa kwenye vituo vya huduma za afya, tunaamini kupitia viongozi hawa wapya wa MSD watakuja na mikakati mizuri ya kutatua changamoto zilizopo na kuhakikisha dawa zinapatikana kwa kiwango kizuri” amesema Mhe. Nyongo

Aidha Kamati imeshauri wataalam wa afya kufanya maoteo sahihi ya mahitaji ya dawa ili kuiwezesha Serikali kufanya manunuzi sahihi ya dawa kulingana na mahitaji yaliyopo.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema katika kipindi hiki cha robo ya kwanza ya Mwaka huu wa Fedha 2022/23 Bohari ya Dawa imeshapokea kiasi cha shilingi Bilioni 40 kwa ajili ya ununuzi wa dawa.

Waziri Ummy amesema kuwa bado kuna maboresho yanafanyika ndani ya MSD na kuhakikisha wanatatua changamoto zilizokuwepo awali ili kuiwezesha MSD kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

“Sambamba na kuweka miundombinu na kuwa na watumishi, kama dawa hakuna, vipimo hakuna, hakuna maana” amesisitiza Waziri Ummy Mwalimu na kuwataka watendaji ndani ya MSD kufanyia kazi changamoto za MSD na kuboresha utendaji kazi.

Bw. Mavere Tukai, Mkurugenzi Mtendaji wa Bohari ya Dawa akiwasilisha taarifa amesema MSD itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutatua changamoto zinzoathiri mnyororo wa ugavi ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.

Bw. Tukai amesema kuwa MSD inahitaji mtaji wa Fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 421 ili iweze kujiendesha yenyewe na kusema kuwa andiko kuhusiana na maombi ya mtaji huo limeshawasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango Mwezi Julai 2022.

“MSD imeendelea kufanya juhudi za kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya huku kwa mwezi Julai hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya muhimu 290 umeborshwa hadi kufikia asilimia 53” amesema Bw. Tukai.

Kuhusu upatikanaji wa dawa za miradi misonge (malaria, kifua Kikuu,/Ukoma Uzazi wa Mpango na Dawa za kufubaza Makali ya Virusi vya Ukimwi) Bw. Tukai amesema kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 dawa zilikuwa zinapatikana kwa wastani wa asilimia 90.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here