Home LOCAL JENGO LA MAMA NA MTOTO HOSPITALI YA KANDA MBEYA KUHUDUMIA WAKINA MAMA...

JENGO LA MAMA NA MTOTO HOSPITALI YA KANDA MBEYA KUHUDUMIA WAKINA MAMA WAJAWAZITO ZAIDI YA 300

Na: Englibert Kayombo WAF – MBEYA.

Kukamilika kwa jengo la kutolea huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kutaongeza idadi ya wakina mama wajawazito wanaofika kujifungua katika Hospitali hiyo kutoka mama wajawazito 150 kwa sasa hadi kufikia 300 kwa wakati mmoja. 

Kauli hiyo imetolewa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Jengo la kutolea huduma za Mama na Mtoto katika Kitengo cha Wazazi Meta.

“Hospitali hii itatoka kulaza wakina mama 150 hadi kufikia zaidi 300 kwa kanda nzima, wakina mama watakaokuwa na hali ngumu pia wataletwa hapa” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema kuwa jengo hilo limewekewa miundombinu ya kisasa ya kuweza kusaidia utoaji wa huduma bora kwa akina mama wajawazito na watoto huku pamoja na kuweka miundombinu ya kuruhusu wanaume kuwepo katika shughuli hiyo ya kuleta kiumbe duniani. 

“Mimi kama mama kazi inayofanywa humu ndani naijua vizuri, naelewa kwamba ni kazi inayohitaji mazingira mazuri sana lakini pia inahitaji faraja na kwa maana hiyo hospitali hii tumeweka vyumba ambavyo mwenza wako atakuwemo humo ndani” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema kuwa Serikali inafanya yote haya ili kuokoa Maisha ya Mama na Watoto huku akisema kuwa uwekezaji huo uliofanywa katika Nyanda za Juu Kusini unafanyika katika maeneo mengine nchi nzima.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka jiwe la msingi katika Hospitali hiyo na kumpongeza Rais Samia kwa kuendeleza kazi walioyoianza toka Awamu ya tano ambapo Serikali ilitoa Shilingi Bilioni 5 kuanza ujenzi wa jengo huku Serikali ya Awamu ya Sita nayo ikiendeleza ujenzi kwa kutoa Shilingi Bilioni 6 kukamilisha ujenzi wa jengo hilo ambalo jumla limeghalimu Shilingi Bilioni 11.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here