Mtwara: 22/08/2022
Huduma za kibingwa za Taasisi ya tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) zitaanza kutolewa katika hospitali mpya na ya kisasa ya rufaa kanda ya kusini Mtwara ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mh. Kanali Ahmed Abbas Ahmed amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kanda Mtwara ambayo itahudumia wakazi wa mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma pamoja na mataifa jirani.
“Pia, nimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface kwa mwitikio wake na kufika Mtwara ili kuona namna bora ya kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mtwara katika kuanzisha huduma za kibingwa za Mifupa katika ukanda wa kusini ili kuwapunguzia wananchi adha ya kufuata huduma hizo Dar es salam”. Alisema Kanali Ahmed
Kanali Ahmed amesema Serikali ya awamu ya sita imetoa fedha kwaajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa katika hospitali hiyo ambapo mtambo wa kisasa wa CT-Scan umeshawasili kwaajili ya usimikaji, mashine ya X-ray imeshasimikwa na mashine ya kisasa ya MRI itawasili hivi karibuni.
Kwaupande wake Katibu tawala wa Mkoa wa Mtwara Mh. Abdallah Malela amesema ujio wa huduma za MOI katika hospitali ya rufaa ya kanda Mtwara utachagiza utalii wa matibabu kwa wagonjwa kutoka mataifa ya Comoro, Msumbiji na hata Malawi.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface amasema MOI inatekeleza kwa vitendo agizo la Mh Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha huduma za kibingwa za Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu zinazogezwa karibu na wananchi ambapo katika mikoa ya kusini tayari huduma za MOI zinapatikana katika hospitali za Nyangao Lindi pamoja na Ndanda