Home LOCAL DKT. MOLLEL AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA VIWANDA VYA DAWA NCHINI

DKT. MOLLEL AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA VIWANDA VYA DAWA NCHINI

 Na: Emmanuel Malegi – DSM

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewakaribisha wawekezaji wa viwanda vya dawa kutoka mataifa mbalimbali kuja kuwekeza nchini kwani fursa hiyo ipo.

Dkt. Mollel amesema hayo leo Agosti 30 2022 wakati alipokutana na wazalishaji na washitiri mbalimbali wa bidhaa za afya wanaoshiriki maonesho ya Kimataifa ya wadau wa bidhaa za afya ya Afrika Mashariki yaliyoanza leo jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mollel amesema hivi sasa Serikali inatafuta njia mbadala ya kupata madawa kwa bei rahisi kutoka viwandani moja kwa moja hivyo uwekezaji wa viwanda hapa nchini utasaidia kuipunguzia Serikali mzigo wa bajeti kubwa ya dawa kama ilivyo sasa kupitia Wizara ya Afya.

“Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshatengeneza mazingira rafiki kwa wafanyabiasha na wawekezaji kuja nchini, wengi wao wameonekana kuvutiwa kuja Tanzania na sisi tutawekea mazingira wezeshi ya kuwafanya wawekeze bila vikwazo. Amesema Dkt. Mollel.

Aidha, Dkt. Mollel ameongeza kuwa dawa ni biashara hivyo amewataka wafanyabishara wa dawa kushirikiana na Serikali ili kudhibiti mfumuko wa bei za dawa nchini ili kuokoa fedha za wananchi na kuwapunguzia mzigo wa gharama za matibabu.

“Serikali imeshaanza mpango wa kununua dawa kwa bei rahisi kutoka viwandani hasa India kwenye wazalishaji wengi, hii itasaidia kupunguza gharama kubwa. Sisi kama Serikali tutaendelea kuwalinda wafanyabiashara wa hapa nchini lakini pia tunaangalia namna ya kuiwezesha bohari ya dawa (MSD) iwe na uwezo wa kununua dawa moja kwa moja kutoka India”. Amesema Dkt. Mollel.

Naibu Waziri Dkt. Mollel akiambatana na Balozi wa India Mhe. Binaya Srikanta walitembelea mabanda mbalimbaali ya Maonesho hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika kwa siku tatu katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar Es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here