DAR ES SALAAM
Waziri wa Malialisili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (MB) ameipongeza amewakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa utoaji wa huduma kupitia mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS) na kuitaka taasisi hiyo kuendelea kushiriki katika maonesho kama hayo ili kukuza uelewa wa wananchi juu ya matumizi ya mfumo huo.
Mhe. Balozi Chana ametoa wito huo mapema leo tarehe 11Julai, 2022 alipotembelea moja ya mabanda ya BRELA yaliyopo katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Wito huo wa Mhe. Waziri unafuatia maelezo yaliyotolewa na Afisa wa BRELA Bi. Mgeni Shaban, baada ya Mhe. Waziri kutaka kufahamu changamoto zilizopo na kuelezwa kuwa baadhi ya wadau hushindwa kurasimisha biashara zao kutokana na kutojua kutumia mfumo huo.
“BRELA muendelee kushiriki katika maonesho haya na mengine ikiwa ni pamoja na kuandaa warsha mbalimbali kwa wadau, juu ya matumizi ya mfumo huu ili kukuza uelewa kwa wananchi wengi zaidi,” amesisitiza Mhe. Balozi Dkt. Chana.
Amesema pia anatambua kuwa taasisi mbalimbali zinashikirikiana na BRELA ili kupata taarifa, pia kama Wizara watahimiza na kuendelea kutumia mfumo wa BRELA kupata taarifa sahihi za makampuni.
Katika Hatua nyingine Mhe. Waziri wamepongeza wadau waliofika katika banda la BRELA ili kurasimisha Biashara zao na kuwataka wakawe mabalozi na kuwahimiza wengine kufika na kupata huduma za BRELA.